Wednesday, January 16, 2013

CHIPOLOPOLO YATAMBA ITATETE UBINGWA


LUSAKA,Zambia

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Zambia,Herve Renard ametamba kuwa,watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanatetea taji lao la ubingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika.

Renard alisema juzi mjini hapa kuwa,wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya fainali za michuano hiyo, zinazotarajiwa kuanza Jumamosi ijayo ikiwa ni pamoja na kucheza mechi nyingi za kujipima nguvu.

"Watu wengi hawaamini kama tunaweza kutwaa tena taji hili na hawataki kuaminisha hisia zao.Ni rahisi kusema kamwe Zambia haiwezi kutwaa tena taji hili,"alisema kocha huyo, ambaye alijijengea heshima kubwa baada ya kuiwezesha nchi hiyo kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka 2012.

 Renard alisema vipigo walivyopata kutoka kwa Tanzania,Saudi Arabia na Angola katika mechi za kirafiki walizocheza hivi karibuni havina maana kwamba kikosi chake ni dhaifu.

Alisema vipigo hivyo vimezidi kuifanya timu hiyo iwe imara na kubaini dosari zilizopo kwenye kikosi chake kwa ajili ya kuzifanyiakazi.

"Iwapo tutashindwa kutetea ubingwa, maana yake ni kwamba timu nyingine ilikuwa bora kuliko sisi. Lakini itakuwa vigumu kuifunga Zambia,"alisema kocha huyo na kuvishutumu vyombo vya habari vya nchi hiyo, ambayo vimekuwa vikikiponda kikosi chake.

Kupona kwa kiungo Rainford Kalaba,aliyekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu, kumempa ahueni kubwa kocha huyo, ambaye pia atakuwa akiwategemea sana kipa Kennedy Mweene, beki Stopila Sunzu na mshambuliaji Christopher Katongo.

Wachezaji wengine nyota wanaotarajiwa kuwemo kwenye kikosi cha Zambia ni beki Emmanuel Mbola, kiungo William Njobvu na mshambuliaji, Jacob Mulenga, ambao walizikosafainali za mwaka 2012 kutokana na kuwa majeruhi.

Zambia imepangwa kundi C pamoja na timu za Ethiopia, Burkina Faso na Nigeria. Itacheza mechi yake ya kwanza Januari 21 mwaka huu kwa kumenyana na Ethiopia. Renard alikiri kwamba,mechi yao dhidi ya Ethiopia ni muhimu kwa vile iwapo watashinda, utakuwa mwanzo mzuri kwao katika kutetea taji hilo.

No comments:

Post a Comment