Saturday, January 19, 2013

CUF YAMILIKI MIGODI MINANE YA MADINI TANGA.



CHAMA cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Handeni, kimekiri kumiliki migodi ya madini minane  mkoani Tanga huku kikiwataka wananchi kupuuza tuhuma zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa hawamiliki kihalali migodi hiyo.
Akihutubia kwenye mkutano wahadhara Katibu wa CUF Wilaya ya Handeni Masoud Mjaila alisema Chama hicho kina Kampuni halali inayomiliki migodi hiyo minane ya madini mbalimbali kwenye Kijiji cha Sezakofi kata ya Ndolwa.
 Huku akionyesha baadhi ya nyaraka za kampuni yao inayomiliki migodi hiyo Mjaila, aliwaonya wakazi wa handeni kuwa macho na wanasiasa wanaohama hama kwenye vyama na kuanzisha vyama vipya kuwa ni watu hatari na wakuogopwa.
 Chama hicho kililazimika kutoa maelezo hayo mbele ya wananchi kufuatia tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na Chama kipya Cha Kisiasa Cha ADC kupitia mlezi wa Chama hicho Doyo Hassan Doyo aliyedai kuwa chama hicho kina miliki migodi bila ya kuwa na vibali.
 “Wananchi msikubali kuburuzwa, hiki chama chenu cha CUF kina miaka 20 tangu kuanzishwa, hapa Handeni kina miaka 15, lakini mnaona hali ilivyo, ndiyo hivi karibuni sasa na sisi tupo ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Mjaila na kuongeza:
 “Sasa hawa ADC wameanza jana, leo wanataka waungwe mkono, hapana! Hawa wanatafuta masilahi yao maana huku CUF walifukuzwa.
 “Eti wanasema migodi ile ya madini haina vibali, siyo kweli kwani serikali iko wapi, tumechangia zaidi ya Sh3.5 milioni, kusaidia miradi mbalimbali ya Serikali ya Kijiji cha Sezakofi.”
 Hata hivyo Chama hicho kilitoa vitu mbalimbali kwa Hospitali ya Wilaya hiyo vikiwemo mashuka  yenye thamani ya Tsh120,000 na sabuni zenye thamani ya Tsh 150,000.
 Mjaila aliwataka wanasiasa kutumia fursa zilizopo kuleta maendeleo nchini kuliko kuendeleza siasa za kupakana matope majukwaani haziwasaidii wananchi

No comments:

Post a Comment