Saturday, January 26, 2013

JAPAN YAIPA TANZANIA BILIONI 28.2 KUBORESHA BARABARA NA KILIMO, MAKUTANO YA TAZARA KUWA NA BARABARA ZA JUU KWA JUU


william_mgimwa
Na Tiganya Vincent-MAELEZO-Dar es salaam
SERIKALI ya Japan imepatia Tanzania msaada wa shilingi bilioni 28.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitatu ya uboreshaji wa usafiri jijini Dar es salaam na kilimo hapa nchini.
Msaada huo umesainiwa (leo) jijini Dar es salaam na Balozi wa Japan hapa nchini Masaki Okada kwa niaba ya Japan na Waziri wa Fedha Dkt. William Mgimwa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kusaini msaada huo Waziri wa Fedha Dkt . Mgimwa alisema kuwa mradi wa kwanza utahusisha upanuzi wa barabara ya Kilwa na ile ya Bandari ambapo jumla ya shilingi bilioni 20 zitatumika katika kukamilisha mradi huo.
Aliongeza kuwa mradi mwingine ni ule wa ujenzi wa barabara za juu(flyover) katika makutano ya TAZARA ambapo jumla ya shilingi bilioni moja (1) na milioni 26 zinatarajiwa kutumika katika kukamilisha mradi huo.
Dkt. Mgimwa aliongeza kuwa eneo lingine ambalo litanufaika na msaada kutoka Japan ni kuunga mkono sera ya Kilimo kwanza ambapo Tanzania imepata shilingi bilioni sita(6) na milioni 92 kwa ajili ya kuhakikisha kunakuwepo kwa usalama wa chakula cha kutosha katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuwa upande wa eneo hilo lengo ni kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wa kipato cha chini wanaboresha kilimo ambacho kitawahakikisha uhakika wa chakula wakati wote na hivyo kuondokana na umaskini.
Kwa upande wa Balozi wa Japan hapa nchini Masaki Okada alisema kuwa wananchi wengi wa Tanzania hasa wakazi wa Jiji la Dar es salaam wamekuwa wakisubiri kwa hamu barabara za juu ili kusaidia kupunguza msongamano wakati wa kuja na kutoka katikati ya jiji la Dar es salaam.
Alisema kuwa utakapo kamilika mradi huo utasaidia kupunguza tatizo la msongamano na hivyo kupunguza saa za mwananchi kusafiri kuja na kutoka katikati ya jiji la Dar es salaam.
Balozi Okada alisema kuwa hatua hii itakuwa muhimu katika kukuza uchumi kwani wananchi watakuwa na muda wa kutosha kuzalisha mali kutoka na miundombinu kuruhusu magari kwenda kasi pasipo kikwazo.

No comments:

Post a Comment