Saturday, January 12, 2013

Kitunda Veteran yafa kiume kwa Wagadau ya Kinondoni



Na Peter Mwenda, Kitunda

TIMU ya Kitunda Veteran jana ilishindwa kutamba mbele ya Wagadau ya Kinondoni baada ya kufungwa mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki wa kujipima ubavu uliofanyika Shule ya  Msingi Kitunda.


Wenyeji wakiongozwa na kipa Lawrance Tigo wakishirikiana na wachezaji Ernest Komba, Henry Kachaso, Allen Msalu, John Tamba, Nico Shimbilu na Lameck Benjamin ilianza mpira kwa kasi na kupigiana pasi fupi fupi lakini haikuwazuia Wagadau kuandika bao la kwanza dakika 24 lililofungwa na Faizi Fatawi baada ya kupokea pasi ya Hassan Mpore "Kiduku".

Mwamuzi wa pambano hilo Erick Sagala aliyechezesha mchezo huo kwa umakini aliruhusu bao la pili kwa timu ya Wagadau lililofungwa dakika ya 52 na Axil Ekatisa aliyepokea pasi ya Kiduku tena aliyekuwa akihaha uwanja mzima kutafuta mabao akisaidiana na mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Ali Yusuf Tigana.

Baada ya bao hilo Kitunda Veteran ilizinduka na kushambulia lango la Wagadau kama nyuki huku washambuliaji wake wakipiga mashuti yaliyoishia mikononi mwa kipa Dulla Abdallah.

Dakika ya 62 Faizi wa Wagadau kwa mara nyingine alifungia timu yake bao la tatu baada ya kupokea pasi ya Kiduku ambaye alionesha kiwango kikubwa katika mchezo huo.Mchezaji huyo anacheza timu ya Magomeni ya mkoa wa Tanga.

Kitunda Veteran ilifanya mabadiliko kwa kuwapumzisha Prime Issa, Mussa Onyango, Faimu Issa, Gitali Marwa na nafasi zao kuchukuliwa na Yahaya Yahaya, Mussa Onyango waliobadilisha sura ya mchezo.

Henry Pablo alifungia timu yake ya Kitunda Veteran bao la kwanza dakika ya 80 baada ya kuwalamba chenga mabeki ya Wagadau baada ya kupokea pasi ya Lameck Mulenda na shuti lake kumpita kipa  Dulla akiwa ameduwaa.

Wakati wakitafakari bao hilo Wagadau walifungwa bao la pili dakika ya 85 kupitia kwa John Tamba aliyepokea pasi ya Henry na kufanya mchezo umalizike kwa Wagadau kutoka kifua mbele kwa mabao 3-2.

Kepteni wa Wagadau,Robert Zullu alisema baada ya mchezo huo kuwa timu ya Kitunda Veteran ni nzuri na kuwashukuru kwa makaribisho mazuri yaliyolenga kujenga udugu kwa wachezaji wa zamani.

Naye Kepteni wa Kitunda, Ernest Komba alisema lengo kubwa la kualika timu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania ni kujenga udugu ambao umeaanza kupotea kwa wachezaji wa zamani waliowahi kuliletea taifa sifa kubwa.

No comments:

Post a Comment