Tuesday, January 15, 2013

ZAIDI YA NCHI 40 KUSHIRIKI KILIMANJARO MARATHON 2013



DAR ES SALAAM, Tanzania

Mbio za Kilimanjaro Marathon mwaka huu zinatajiwa kuwa na washiriki wa kigeni wapatao 600 kutoka nchi zaidi ya 40.

John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa mbio hizo zinaendelea kuwavutia washiriki wengi wa kimataifa kutokana na jitihada za pamoja zinazofanywa na waandaaji pamoja na bia ya Kilimanjaro Premium Lager katika kutangaza tukio hili. Hii ndi sababu iliyochangia ukuaji wa mbio hizi pamoja na ushiriki kuongezeka kila mwaka.
Addison alisema washiriki wengi zaidi watatoka Marekani ikifuatiwa na Uingereza. Nchi nyingine zinazotarajiwa kushiriki ni pamoja na Canada, Japan, Uganda, Zimbabwe na Kenya. Nyingine ni pamoja na Sweden, Australia, Hungary, Germany,  Zambia, Morocco, Swaziland, Nigeria na Malawi.

Zikiwa zimepangwa kufanyika Moshi tarehe 3 Machi 2013, mbio za Kilimanjaro Marathon zitakuwa zimegawanyika katika sehemu nne ambazo ni 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon,  21km Half Marathon, GAPCO Disabled Half Marathon na Vodacom 5km Fun Run.

Mbio hizo pia zinatarajiwa kuchangamshwa na ushiriki wa timu za makampuni ambapo wafanyakazi wa makampuni wadhamini watashindana katika mbio ya nusu marathon kupitia shindano litakalojulikana kama“Half Marathon Corporate Challenge”. 

Makampuni ambayo yameishathibitisha kushiriki shindano hilo ni pamoja na TPC Sugar ambao ndio mabingwa watetezi wa shindano hilo wakifuatiwa na CFAO Motors, TanzaniteOne na Tanga Cement.

Addison alisema kuwa mbio za Kilimanjaro Marathon zinaingia katika mwaka wa 11 tangu kuanzishwa zikiwa zimesajiriwa rasmi na shikisho la riadha la kimataifa na kuongeza kuwa kutakuwepo na vituo vya maji pamoja na viburudisho katika njia ya mashindano hayo.

“Mbio hii inafanyika chini ya Mlima Kilimanjaro ambapo kila mtu anaweza kukimbia kwa raka kwani urefu wake kutoka usawa wa bahari ni wastani wa mita 830 mpaka 1150 katika barabara nzuri yenye lami. Inatarajiwa kuwa shamrashamra maana wananchi wengi  watajitokeza pembezoni mwa barabara kuwashangilia na kuwapa moyo wakimbiaji, na wakimbiaji wa kujifurahisha wanaweza hata kusimama kupata kiburudisho njiani”, Addison aliitimisha.

Mbio hizo zinadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager (wadhamini wakuu), Vodacom Tanzania (5km Fun Run), GAPCO (Disabled Half Marathon), Tanga Cement, CFAO Motors, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, New Arusha Hotel na Kilimanjaro Water.

No comments:

Post a Comment