Friday, February 15, 2013

BUNGE LAOGOPA SAUTI ZA WANANCHI NA KUKUBALI VIKAO VYOTE KURUSHWA LIVE


JAMHURI YA MUUNGANO WATANZANIA

BUNGE LA TANZANIA

__________

TAARIFA MAALUM KUHUSU BUNGE NA KAMATI


Ofisi ya Bunge imepokea kwa masikitiko taarifa kuhusu tafsiri ya kusitisha matangazo ya Shughuli za Bunge na Kamati, kinyume na jinsi ilivyoakisiwa katika mazungumzo ya pamoja kati ya Wanahabari na Katibu wa Bunge. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, Bunge la Jamhuri ya Muungano halina mpango wa kusitisha matangazo ya Bunge wala Kamati zake, ambazo kwa mahitaji ya sasa nazo zinapaswa kurushwa moja kwa moja kama sehemu ya mpango kabambe wa kuwapasha Wananchi yanayojiri katika Uendeshaji bora wa Shughuli za Bunge.Dhamira ya Bunge ni kuhakikisha kuwa mpango kabambe uliopo ni kumfikia kila Mtanzania alipo na kwa uwezo alionao aweze kupata na kushiriki katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. 


Hivyo Mpango mkakati uliopo utakuwa kuboresha mawasiliano ya kawaida kupitia Teknolojia ya Mawasiliano TEKNOHAMA, kwa wale watakaokuwa na uwezo wa kupata huduma za mtandao, na tayari tumeanza kurusha live video striping kupitia tovuti ya Bunge, na hata wale watakaopenda kujua zaidi, basi wanaweza kupitia majadiliano ya Bunge kwa nyakati tofauti. Aidha, kwa wale watakaokuwa na uwezo wa kushika mawimbi ya Radio, basi wataweza kufuatilia majadiliano ya Bunge katika Radio ya Bunge inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni katika masafa yanayoweza kupatikana nchi nzima, hii ikiwa ni jitihada za ziada kwa kuwa kuna Radio zinazotoa huduma hiyo ya moja kwa moja vizuri hadi sasa, kama vile RTD,BBC, STAR etc. Aidha, kwa wale watakaoweza kuwa na uwezo wa kumudu Luninga, basi Bunge limejipanga kuwapatia huduma hiyo moja kwamoja kupitia katika mtandao wake mpya utakaokuwa ukirushwa masaa 24, baada ya mitambo mipya ya kunakili majadiliano Bungeni na katika Kamati kusimikwa.

Hivyo basi utaratibu uliopo sasa utaendelea kutumika ambapo vituo vyote vya Television vitapewa fursa ya kurusha matangazo kwa utashi wao bila kuwekewa mipaka ya aina yoyote sambamba na matangazo yatakayotolewa na mitandao ya Bunge. Utaratibu huu unatokana na uamuzi wa pamoja kati ya Bunge na Tume ya Mawasiliano, ambapo vipindi vyote vya Bunge vitakuwa vinarushwa bila kudhaminiwa na taasisi yoyote zaidi ya mamlaka tajwa juu ya mawasiliano TCRA. Hivyo basi kwa maelezo hayo ni dhahiri kuwa Bunge halina mpango wa kusitisha matangazo ya TV wala yale ya Radio au Teknohama, bali linatarajia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa utaratibu ulio rahisi na unaoweza kusimamiwa na pande zote, yaani Bunge na Wananchi. Aidha, kwa utaratibu uliopo sasa,Bunge halirushi matangazo ya aina yoyote, bali hutoa nakala ya majadiliano hayo kwa mtu yeyote atakaye au TV na Radio yoyote kupitia katika mitambo yake. TV zote zinazorusha matangazo ya Bunge hupata feed toka katika mitambo ya Bunge, na pale wanapoona yafaa basi huomba kutumia mitambo yao na hivyo kutumia fursa hiyo kuingiza Camera na Wanahabari ndani ya ukumbi wa Bunge kwa minajiri hiyo. Kuzingatia mabadiliko tajwa, utaratibu huo umepewa ukomo, ili sasa hapatakuwa na fursa ya kuingiza Camera ndani ya Kumbi za Bunge, bali wote watakaotaka kurusha matangazo ya Bunge kwa utashi wao, watapata clear feed toka katika mitambo ya Bunge na hivyo kurusha live vipindi vyote vya Bunge bila kuhaririwa kama ilivyonakiliwa katika makala mbalimbali.

Hata hivyo utaratibu huu wa kutumia Camera katika Kumbi utaendelea katika Kamati za Bunge, hadi hapo mitambo mipya ya mawasiliano itakapofungwa katika Kumbi zote za Kamati. Hivyo basi, ili kwenda sawia na taratibu hizo, Bunge litaendesha zoezi la kuwatathmini Waandishi wote wa habari za Bunge na kuwasajili kwa vigezo vitakavyoafikiwa kati ya Baraza la Habari,Idara ya Habari na Bunge lenyewe. Aidha ili kulinda heshima na maadili ya utangazaji, Bunge litatoa utaratibu (Code of Conducts for Media broadcasting) wa namna ya kunakili na kurusha matangazo ya Bunge bila kujali yanarushwa kwa utaratibu upi. Hili litasaidia kuweka misingi bora ya mawasilaino na hivyo kuwapa fursa Wananchi kujua hali halisi ya matukio yote ndani ya Bunge na katika Kamati, bila kuegemea upande wowote (Non Partisan). Hivyo basi, wakati zoezi la maboresho hayo likiendelea, Wananchi watajulishwa kila hatua na matarajio tajwa na kwamba tunaendelea kusisitiza tena, Wananchi wasiwe na hofu juu ya taarifa zilizopewa uzito usio stahili za kusitisha matangazo ya Bunge, ambao hazikuwa sahihi na pia hazikuainisha zoezi zima la maboresho ya upatikanaji na usambazaji wa habari za Bunge. Tunasikitika kwa usumbufu uliowasibu wote walioakisiwa na taarifa hiyo.


Dr. Thomas D.Kashililah

KATIBUWA BUNGE

No comments:

Post a Comment