Friday, March 29, 2013

MALKIA WA NYUKI AHIMIZA WATOTO KUIPENDA SIMBA SC


 Malkia akimvalisha jezi mmoja ya watoto wanaolelelewa kituoni hapo

Baadhi ya watoto wanaolelewa kwenye kituo cha Umra wakiwa wamevalia jezi za Simba baada ya kukabidhiwa na Malkia wa Nyuki

MFADHILI  wa timu ya soka ya Simba Rahma Al Kharous ‘Malkia wa Nyuki’, ameanza mikakati ya kuandaa wachezaji chipukizi  ikiwa ni sehemu ya mkakati wa timu ya Simba kuanza kutayarisha hazina ya wachezaji wa baadaye.
Tukio hilo lilifanyika  juzi kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha Umra kilichopo Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam alipokwenda kukabidhi vifaa vya michezo pamoja na mahitaji mengine ya kibinadamu ikiwemo mchele, mafuta, sukari, sabuni, unga sambamba na kula pamoja na watoto hao chakula alichoandaa kwa ajili yao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Al Kharous ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya  Simba alisema ameamua kuwapelekea jezi hizo ili kuanza kuwahamasisha mapema watoto hao kuipenda michezo na zaidi klabu ya Simba.
“Nimefanya hivi ili kuunga mkono kauli ya Rais wetu Jakaya Kikwete wa kuanza kuwekeza katika timu za watoto, napenda watoto muipende Simba ili mje kuichezea mtakapokuwa wakubwa na hatimaye kupata nafasi ya kuichezea pia timu yetu ya Taifa,”alisema
Malkia ambaye jezi alizokabidhi kwa mbele ziliandikwa I Love Simba FC na kwa nyuma ziliandikwa Malkia , aliongeza kwamba viongozi wa Simba wako makini katika mkakati wa kuanza msingi wa kuandaa wachezaji chipukizi kwa ajili ya manufaa ya timu yao katika siku za usoni.
“Huu ni mkakati tuliojiwekea na hatutaishia hapa, kwani tumedhamiria kufanya mambo makubwa katika mkakati huu wa kuandaa wachezaji kuanzia hatua za chini na kisha mambo mengine yatafuata,”aliongeza
Aidha, Malkia alisema kwa sasa wanataka kufanya kazi za kijamii zaidi ili watu na hasa watoto waifahamu zaidi Simba kuwa ni timu ya kuendeleza soka na si malumbano.
Mbali na hayo, Malkia alisema jukumu la kulea ama kusaidia watoto yatima ni la kila mtu na si kwa watu wenye fedha tu, hivyo amehimiza watu wengine kujitokeza kusaidia kwani kwa kufanya hivyo watapata thawabu kutoka kwa mwenyezi mungu.
“Hakuna mtu anayependa kuwa yatima, mimi nilimpoteza mama yangu mzazi nikiwa mtoto mdogo lakini sikukata tamaa mpaka nikafikia hapa ambapo nina uwezo wa kutosha na hivyo natumia nilichonacho kuwasaidia na wengine kama ninyi,”alisema
“Msijisikie unyonge kwa kuwa yatima muombeni mwenyezi mungu na kujituma bila kuchoka, naamini ipo siku mtakuwa watu fulani katika jamii yetu,”aliongeza
Aidha, Malkia aliahidi kuhakikisha anasaidia kumalizi ujenzi wa kituo cha watoto hao kilichopo Mbezi Msakuzi na kusema atalifanya hilo kwa uharaka zaidi ili kuwawezesha watoto hao kuishi sehemu itakayowapa na nafasi ya kutosha, pia kuwezesha uongozi kuepukana na masuala ya kodi ya pango la nyumba.
“Nitakuwa pamoja nanyi katika kulitekeleza hili, naamini mkiwa na sehemu yenu itakuwa vizuri zaidi kupunguza gharama za ziada, pia watoto watapata nafasi ya kutosha,”aliongeza.
Awali, akisoma risala ya kituo hicho, mmoja ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho, Ashraf Muzamil alisema kwamba, kituo hicho kilianzishwa mwaka 2003 kikiwa na watoto saba lakini mpka sasa kina watoto 67.
Alisema, kituo hicho kimekuwa mstari wa mbele  kuwasaidia watoto yatima kujiepusha na mambo maovu yakiwemo ulevi, uvutaji bangi na mengineyo yasiyofaa.
Hata hivyo, Ashraf alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mavazi, ada kwa watoto wanaosoma, malazi n.k, hivyo uongozi umekuwa ukihangaika kutafuta wafadhili ili kusaidia.
Ashraf pia alimshukuru Malkia kwa kuwatembea kituoni hapo pamoja na kutoa misaada ya hali mali, huku akimtakia maisha marefu zaidi ZAID TEMBELEA http://dinaismail.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment