Tuesday, March 26, 2013

Mke wa Rais wa China Mama Peng Liyuan aipongeza WAMA


Mama Peng Liyuan
Na Anna Nkinda – Maelezo

Mke wa Rais wa China Mama Peng Liyuan   amezipongeza kazi  zinazofanywa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kupitia taasisi anayoiongoza ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ya kuhakikisha kuwa inawainua wanawake kiuchumi na kuwasaidia  watoto wa kike ambao ni yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi kupata  elimu sawa na watoto wengine.

Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati Mama Liyuan alipotembelea ofisi ya WAMA kwa ajili ya kuona kazi mbalimbali wanazozifanya  na  kutoa zawadi ya vyerehani 20 kwa ajili ya Umoja wa Vikundi vya WAMA  (UVIMA) na mabegi ya shule 100 kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama.

Mama Liyuan alisema kuwa  kupitia taarifa mbalimbali alizozisoma ameweza kufahamu  kazi na juhudi za Mama Kikwete anazozifanya za kuisaidia jamii na ataangalia jinsi gani anawezea kumuunga mkono kutokana na kazi anazozifanya.

Kwa upande wake Mama Kikwete alimpongeza Mama Liyuan  kwa kuitembelea  Tanzania muda mfupi mara baada ya mume wake  kuwa madarakani  kwani kitendo hicho kinaendeleza  ushirikiano na urafiki uliopo baina ya Tanzania na China ambao upo kwa miaka mingi.

“Ninaomba tuendelee kushirikiana kutatua matatizo yanayowakabili wanawake na watoto wa kike kwani changamoto zao zinafanana Duniani kote na  umuhimu wa kuzifanyia kazi ni uleule”, alisema Mama Kikwete.

Naye Tatu Ngao ambaye ni Mwenyekiti wa UVIMA ambao umepata zawadi za vyerehani 20 vya kudarizi alishukuru kwa vyerehani walivyopewa na kusema kuwa vitawasaidia kuongeza ujuzi, kuinua kipato chao na hivyo kujikwamua kiuchumi.

Alisema kuwa ndani ya UVIMA kuna  jumla ya vikundi vya maendeleo 35 ambavyo ni mchangiko wa wanaume na wanawake ila asilimia kubwa ya wanachama wake ni wanawake kutoka kata ya Majohe Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Ngao alisema, “Jambo la muhimu ni  wanawake wajiunge katika vikundi vya maendeleo na wahakikishe kuwa vikundi hivyo vimesajiliwa ili waweze kufikika kirahisi na kujikwamua kiuchumi kwani sisi bila kuwa katika vikundi tusingeweza kupata  misaada mbalimbali tunayopewa”.

Akiongea kwa niaba ya wenzake Winfrida leonard ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama ambayo iko Nyamisati wilayani Rufiji alishukuru kwa zawadi ya mabegi waliyopewa na kusema kuwa yatawasaidia kutunza madaftari kwani wanahitaji kuwa na mabegi.

“Ninaishukuru Taasisi ya WAMA kwa kutusaidia kielimu kwani tunasoma bure  bila ya kuchangia kiasi chochote cha fedha na tunapata mahitaji yote ya muhimu kama chakula, maladhi na mavazi.

 Ninaiomba  Serikali iweze kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ambao wamekosa nafasi ya kusoma kwa kuwakusanya pamoja na kuwapa elimu kama alivyofanya Mama Kikwete kwani watoto ni taifa la kesho”, alisema Leonard.

Mama Peng Liyuan ameambatana na mumewe Rais Xi Jinping nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

No comments:

Post a Comment