Sunday, April 14, 2013

Barabara katika Maeneo ya Iyunga Viwandani kutotekelezwa na ngazi husika madhara yaanza kutokea baada ya magari kuanza kuanguka yakiwemo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya


Gari la kiwanda cha Cocacola likiwa limepinduka (Picha na Mbeya Yetu)
Nalo gari la halmashauri ya jiji limekwama
Hii ndio barabara ya Viwanda Iyunga jinsi ilivyo


SIKU chache baada ya Mbeya yetu kuripoti habari kuhusu baadhi ya Wananchi kulalamikia ubovu wa Barabara katika Maeneo ya Iyunga Viwandani kutelekezwa na ngazi husika madhara yaanza kutokea baada ya magari kuanza kuanguka yakiwemo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya.


Baadhi ya barabara zinazo lalamikiwa na wananchi hao ni ile inayo toka eneo la Ituta Iyunga ambayo inaelekea katika viwanda vya makampuni ya Cocacola, Pepsi, Tbl, pamoja na kiwanda cha utengenezaji malumalu(Marmo granite limited).
  
Wakizungumza na Mbeya yetu kwa sharti la kutotaja majina yao wananchi hayo walisema barabara zinazo elekea viwandani humo ni mbovu na hazina hadhi ya kutumiwa na makampuni hayo.
  
Walisema kutokana na hali hiyo hawaoni mchango na umuhimu wa uwepo wa makampuni makubwa maeneo yao kutokana na kushindwa kuhudumia barabara ambazo wanapitisha bidhaa zao wenyewe.
  
Aidha wameziomba mamlaka husika jijini humo kuhakikisha wanayafanyia kazi malalamiko hayo kwani ni kero kubwa hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua.
  
Baadhi ya madereva wanaopita na magari ya mizigo kutoka viwandani walisema magari yao hushindwakumudu kutokana na ubovu wa miundombinu hiyo licha ya kutoa ushuru mkubwa kwa halmashauri ya Jiji.
  
Walisema baadhi ya bidhaa wanazokuwa wamezibeba haziitaji mtikisiko mkubwa kutokana na kupoteza ubora wake hivyo wakiendelea kupita kwenye barabara hizo kampuni hupoteza wateja kutokana na bidhaa kupoteza ubora.
  
Baadhi ya Magari yalioanza kupata madhara kutokana na ubovu wa barabara hizo ni Gari inayomilikiwa na Kampuni ya Cokacola yenye namba za usajili T 781 ALL, yenye Tela namba T 168 ALD likiendeshwa na dereva Medson Msisya pamoja na Gari ya Halmashauri ya Jiji lenye namba SM 2732 lililokuwa likienda kunyonya maji machafu katika Barabara hiyo hiyo ya Viwandani.
  
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Juma Iddi alipoulizwa kuhusu barabara hizo alisema Makumpuni hayo yana ubishi kwa kushindwa kufanya ushirikiano na Halmashauri ya Jiji ambayo tayari imeshaanza kukarabati baadhi ya maeneo.

Alisema barabara hiyo ipo kwenye kiwango cha vumbi hivyo kutokana na kupitika mara kwa mara na makampuni hayo inabidi ipandishwe ili ijengwe kwa kiwango cha changarawe ili zipitike kipindi chote cha Mwaka.
  
Iddi alisema kutotengenezwa kwa barabara hiyo kwa sasa kumetokana na kukosekana kwa fedha ambazo hutegemea kutoka kwenye mfuko wa barabara pamoja na fedha za halmashauri.

Pia alisema kwa sasa Halmashauri hiyo inasubiri fedha za mabaki kutoka Mfuko wa benki ya dunia ambazo zinakarabati  Barabara za Jiji kwa kiwango cha Lami.

No comments:

Post a Comment