Wednesday, April 3, 2013

Extra Bongo kunogesha Media Day


Wanamuziki wa Extra Bongo wakiwajibika
BENDI ya Extra Bongo imeahidi kuwaburudisha vilivyo waandishi wa habari wanaotokea katika vyombo mbalimbali vya habari katika tamasha la Media Day linalotarajiwa kufanyika Jumamosi.
Kwa mujibu wa kiongozi wa bendi hiyo, Rogert Hegga, Extra Bongo imefurahi kuteuliwa kutoa burudani kwenye tamasha hilo na hasa kwa kuzingatia kwamba ni mara yao ya kwanza.
Tamasha hilo limendaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), litafanyika kwenye viwanja vya TCC Club Chang'ombe jijini Dar es Salaam, ambapo litashirikisha michezo mbalimbali.
"Tumejiandaa kuwapa burudani ya kutosha kwa sababu tuna nyimbo nyingi tu zikiwamo za albamu Extra Bongo ya mwanzo na sasa na pamoja na nyimbo nyingine zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu mpya," alisema Hegga.
Kiongozi huyo alisema kuwa TASWA hawakukosea kuiteua Extra Bongo, kwa madai kwamba wamesoma ishara za nyakati na kutambua kuwa ndiyo bendi yenye mashabiki wengi kwa sasa.
"Kwa kujali jinsi walivyotuthamini na kutupendekeza kutoa burudani kwenye tamasha lao, hatuna budi kuwapa kile ambacho kitawafanya watualike kila wanapofanya matamasha yao," alisema.
Bendi hiyo kwa sasa ina albamu za 'Mjini Mipango' na 'Mtenda Akitendeewa', ambapo pia imekamilisha nyimbo mbili mpya za 'Mgeni' na 'Hafidh' ambazo zinasikika kwenye maonyesho ya bendi hiyo.

No comments:

Post a Comment