Na Kambi Mbwana,
Dar
es Salaam
MRATIBU wa mashindano
ya riadha ya Ruaha Marathon, Albert Sanga, amesema kwamba wanaendelea na
maandalizi yao kwa ajili ya kufanyika kwa mashindano hayo kwa ufanisi na
kukutanisha watu zaidi ya 2500 mkoani Iringa, hapo Mei 25.
Ruaha Marathon
yamepangwa kutimua vumbi mkoani Iringa, huku wanariadha kutoka ndani na nje yaa
nchi wakitarajiwa kuonyeshana uwezo huku dhima kubwa ya mashindano hayo ikiwa
ni kukuza sekta ya utalii wa ndani hapa nchini.
Akizungumza kwa njia
ya simu kutoka mkoani Iringa, Sanga alisema kwamba wamekuwa wakifanya juhudi za
hapa pale ikiwa ni kuwasiliana na wadau namna ya kuandaa mashindano yenye mguso
na malengo makubwa kwa sekta ya riadha.
Alisema kuwa Ruaha
Marathon ni kwa ajili ya Watanzania wote, huku lengo lingine ni kukusanya fedha
za kuwasaidia watoto walemavu, hivyo wanaamini wakifanikisha mbio hizo kila
sekta itafanikisha, sambamba na kukuza utalii.
“Ruaha Marathon
tunataraiia kushirikisha watu kutoka Italia, Canada, Marekani, Uingereza,
Australia, Kenya, Ethiopia, Afrika Kusini na nchi nyingine, hivyo kwasababu hii
lazima waandaaji tupigane kadri ya uwezo wetu kwa ajili ya kufanikisha lengo
letu.
“Naamini mambo
yatakuwa mazuri kwa kuona kuwa tunafanikisha mashindano haya kwa kiwango cha
juu na kuendeleza sekta ya michezo pamoja na kutangaza utalii wetu ambao kwa
hakika utakuwa na tija kwa namna moja ama nyingine,” alisema.
Kwa mujibu wa Sanga,
watu wa kada mbalimbali, wakiwamo mawaziri, wabunge na wengineo nao watakuwapo
kwenye mashindano hayo kuangalia kila kitakachojiri kwa siku hiyo maalum ya
Ruaha Marathon mkoani Iringa.
No comments:
Post a Comment