Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
mchezaji wa zamani wa timu za Coastal Union, TPC na Taifa Stars, Behewa
Ali Sembwana (72) kilichotokea jana usiku (Machi 31 mwaka huu) mkoani
Tanga.
Msiba
huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti
Sembwana akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali
alizochezea, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
Sembwana
aliyekuwa akicheza wingi ya kulia alidumu katika Taifa Stars kwa miaka
kumi, kama ilivyokuwa kwa kombaini ya Mkoa wa Tanga (Tanga Stars)
aliyoiwakilisha katika michuano ya Kombe la Taifa (Taifa Cup).
TFF
inatoa pole kwa familia ya marehemu Sembwana, Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal Union na kuwataka kuwa na
subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko
yanatarajiwa kufanyika leo (Aprili 1 mwaka huu) kijijini kwake Lusanga,
Wilaya ya Muheza mkoani Tanga. Mungu aiweke roho ya marehemu Sembwana
mahali pema peponi. Amina
WALIBERIA WA AZAM KUWASILI KESHO
Timu
ya Barrack Young Controllers II ya Liberia inatarajia kuwasili nchini
kesho (Aprili 2 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la
Shirikisho dhidi ya Azam itakayochezwa Jumamosi (Aprili 6 mwaka huu)
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Young
Controllers itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) saa 3.35 asubuhi kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Nairobi,
Kenya inapounganisha safari hiyo inayoanzia Monrovia kupitia Accra,
Ghana.
Msafara
wa timu hiyo utakuwa na watu 37 wakiwemo wachezaji 21 na utaongozwa na
Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo Robert Alvin Sirleaf ambaye ni
mtoto wa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf.
Wachezaji
waliomo kwenye kikosi hicho ni Abraham Andrew, Alfred Hargraves, Alpha
Jalloh, Benjamin Gbamy, Cammue Tumamie, Erastu Wee, Ezekiel Doe, George
Dauda, Hilton Varney, Ishmail Paasewe, Joekie Solo, Joseph Broh, Junior
Barshall, Karleo Anderson, Mark Paye, Prince Jetoh, Prince Kennedy,
Randy Dukuly, Raymond Blamonh na Winston Sayou.
Benchi
la ufundi linaongozwa na Kocha Mkuu Robert Lartey akisaidiwa na Samuel
Sumo wakati Meneja wa timu ni Clarence Murvee. Daktari wa timu ni Samuel
Massaquoi.
Timu
hiyo inatarajia kundoka kurejea Monrovia, Aprili 8 mwaka huu kupitia
Nairobi, Kenya saa 11.10 alfajiri kwa ndege ya PrecisionAir.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI WA POLISI TABORA
Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za
kifo cha mshambuliaji wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ya Polisi
Tabora, Regan Mbuta kilichotokea jana (Machi 31 mwaka huu) usiku kwa
ajali ya pikipiki mjini Tabora.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora
(TAREFA), Yusuf Kitumbo, marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo (Aprili 1
mwaka huu) kwenda kijijini kwao Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani
Morogoro kwa ajili ya maziko.
Msiba
huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mbuta alikuwa mmoja wa
washambuliaji tegemeo wa Polisi Tabora, na bao lake la mwisho
aliyoifungia timu ilikuwa kwenye mechi ya mwisho ya FDL msimu huu dhidi
ya Pamba ya Mwanza iliyochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF
inatoa pole kwa familia ya marehemu Mbuta, TAREFA na klabu ya Polisi
Tabora na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Mbuta mahali
pema peponi. Amina
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment