Wednesday, April 17, 2013

UJUMBE WA FIFA ULIOKUJA NCHINI KUSIKILIZA MGOGORO WA UCHAGUZI WAZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI


Mkurugenzi wa Wanachama wa shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Primo Corvaro akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu hatma ya mgogoro wa wagombea na shirikisho la Soka nchini (TFF) ambao ulisababisha mchakato wa uchaguzi kusimama. 







HATMA ya wagombea sita walioenguliwa kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), sasa itajulikana baada ya wiki moja.
Hatua hiyo imekuja baada ya wajumbe wa Fifa kurejea Uswisi, ambako watatuma hatma ya wagombea hao kwa TFF na maelekezo mengine.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Idara ya Uanachama wa Fifa,  Primo Carvaro, alisema wamefanya mahojiano na wagombea wote waliokuwa wanalalamika, hivyo watarudisha majibu hayo baada ya wiki moja.
“Muda tuliokuwa nao ni mdogo sana, hivyo tumechukua malalamiko yao na tunakwenda nayo Uswisi ambako ndiko hatima ya uchaguzi huo itakapojulikana,” alisema.
Alisema uchunguzi waliofanya wamegundua Tanzania kuna changamoto nyingi, ikiwa sambamba na kuwa na wapenzi wengi wa soka.
“Hii ni hazina kubwa sana, hivyo tuna imani kama wakiwa wavumilivu basi wataipeleka nchi yao mbali, hasa katika michuano ya kimataifa,” alisema.
Primo alisisitiza kuwa iwapo FIFA itabaini mwanachama kwenda mahakamani basi watatumia sheria iliyowekwa kuifungia Tanzania.
“Suala hili hatutakuwa na msamaha nalo, kwani lipo ndani ya kanuni ya FIFA, hivyo kama tukibaini kuwa wamekwenda mahakamani basi tutawafungia,” alisema.
Alisema hatima ya viongozi hao ni ndogo sana, kwani haitachukua hata karatasi moja itakayotumwa nchini.
Primo aliongeza licha ya kupata nafasi ya kusikiliza watu hao, alisema wao kama wao hawana majibu rasmi ya kutatua tatizo hilo hadi pale watakapopata nafasi ya kukutana na sekretarieti ya CAF na FIFA, ili kutoa majibu sahihi juu ya tatizo hilo.
Alisema mara baada ya kuondoka wao, FIFA itatuma makachero wake ambao watakuja kuchunguza kwa kina kile walichokisikia, ili kujua ukweli juu ya jambo hili ambalo linahatarisha ustawi wa mpira hapa nchini.
Ofisa Maendeleo wa Fifa Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi, aliwataka waandishi wa habari kuwa makini ili kutoiingiza nchi yao katika matatizo.
“Waandishi ndio wanaoweza kuikuza TFF au kuizamisha, hivyo wanatakiwa kuwa makini katika kazi zao,” alisema.
Wakati huo huo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga, alisema wajumbe hao wa FIFA wameweza kukutana na viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na  Michezo, chini ya Katibu wake Seith Kamuhanda sambamba na Mkurugenzi wa  Idara ya Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo.
“Waziri Fenela Mukangara hayupo, amesafiri na Naibu wake Amos Makalla yupo bungeni, hivyo ujumbe huo ulikutana na Thadeo na Kamuhanda ambapo kwa sasa tunasubiri muongozo kutoka FIFA ili kuendelea na uchaguzi huo,” alisema.
Wagombea ambao hatima yao ipo mikononi mwa Fifa ni Jamali Malinzi, Michael Wambura, Hamad Yahaya, Eliud Mvela, Farid Nahd na  Mbasha Matutu.
Awali ujumbe huo wa Fifa ulifanya kikao na sekretarieti ya TFF kuanzia asubuhi mpaka saa tano, ambapo iliingia kamati ya uchaguzi chini ya Deogratius Lyato.
Wagombea sita walikuwa kwenye viunga vya hoteli ya Serena kulipofanyika kikao hicho tangu saa tano asubuhi hadi saa tisa.

No comments:

Post a Comment