Monday, June 24, 2013

Azimo la Mazingira bora na salama kwa waandishi wa habari wakiwa kazini lazinduliwa leo jijini Dar es Salaam


IMG_2565
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa Tamko la Mount Meru la kuwalinda waandishi wa habari wakiwa kazini Afrika Mashariki, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Bw. Francis Stolla akizungumza machache wakati wa uzinduzi huo ambapo alisisitiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari katika kujenga Demokrasia na Utawala Bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kati. Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Misa-Tan Bw. Mohammed Tibanyendera (wa tatu kushoto), Mjumbe wa MCT Bw. Allan Lawa (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Bw. Abubakar Karsan ( wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa MISA-TAN Bw. Tumaini Mwailenge (kushoto). 
IMG_2504
Mtangazaji wa Radio Clouds Fm Regina Mwalekwa akisoma Tamko rasmi la Mount Meru lililoandaliwa siku ya maadhimisho ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani yaliyofanyika Mei 3-4 mwaka huu jijini Arusha yaliyohudhuriwa na washiriki mbalimbali toka vyombo vya habari, redio za jamii, jumuiya mbalimbali za Kimataifa, Taasisi za mafunzo ya tasnia ya habari na mifuko ya Maendeleo ya Tasnia ya habari kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda.
IMG_2519
Mgeni rasmi Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Bw. Francis Stolla (wa pili kulia) akizundua rasmi Tamko la Mount Meru linalozunngumzia vipengele mbalimbali vitakavyowalinda waandishi wa habari Afrika Mashariki.
IMG_2533
Mgeni rasmi Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Bw. Francis Stolla akionyesha Tamko rasmi la Mount Meru la kutetea Uhuru wa Vyombo vya Habari kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.
IMG_2543
Mgeni rasmi Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Bw. Francis Stolla akizindua rasmi CD ya wimbo ulioimbwa na Mjomba Band unaoitwa "Uhuru Wangu" uliopigwa kwa mara ya kwanza wakati maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika katika Hoteli ya Naura Springs jijini Arusha. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mwenyekiti wa Misa-Tan Bw. Mohammed Tibanyendera ( wa pili kushoto), Mjumbe wa MCT Bw. Allan Lawa (kulia) na Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Bw. Abubakar Karsan (kushoto).
IMG_2550
Sasa umezinduliwa rasmi....Kaa tayari kuusikiliza katika radio mbalimbali na mitandao ya kijamii hapa nchini.
IMG_2490
Mjumbe wa MCT Bw. Allan Lawa akizungumza umuhimu wa waandishi wa habari kujali maslahi mapana ya taaluma ya uandishi wa habari katika mchakato wa kuandika Katiba mpya kupitia mabaraza ya Katiba ya Wilaya.Vile vile alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kushiriki kikamilifu katika kujadili rasimu ya Katiba mpya iliyozinduliwa hivi karibuni na Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal ili kuhakikisha Taifa linapata Katiba Mpya inayojali Uhuru wa vyombo vya Habari hapa nchini.
IMG_2595
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Bw. Abubakar Karsan akifafanua jinsi Mfuko wa Mwangosi utakavyokuwa ukisaidia waandishi wa habari wanaopata majanga wakiwa kazini vile vile utaenda sambamba na Tuzo ya Mwandishi ambaye atakuwa amepata matatizo, misukosuko katika kutafuta habari za uchunguzi na Tuzo hiyo itakuwa ikitolewa kila mwaka Septemba 6 siku aliyokufa Daudi Mwangosi na mshindi atajinyakulia Milioni 10 zitakazotolewa na waendeshaji wa mfuko huu UTPC.
IMG_2497
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania Jane Mihanji akiteta jambo na Usia Nkhoma Ledama wa Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) (Wa pili kushoto) na Bi. Rose Mwalimu kutoka UNESCO (wa pili kulia).
IMG_2585
Mdau kutoka Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) akitoa maoni yake juu ya tamko la Mount Meru kwenye uzinduzi uliofanyika leo jijini Dar katika Hoteli ya Peacock.
IMG_2575
Baadhi ya waandishi wa habari waandamizi nchini kutoka kushoto ni Shermax Ngehemera Mhariri wa The African, Hamis Mzee wa MCT na Mhariri wa zamani wa Mwanaspoti ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa TFF Angetile Osiah.
IMG_2495
Wadau mbalimbali kutoka kwenye vyombo vya habari waliohudhuria uzinduzi wa tamko la Mount Meru.
--
Kufuatia Mkutano wa Wadau wa Habari Afrika Mashariki waliadhimia yafuatayo;-
1.Serikali zote nchi za Afrika Mashariki zihakikishe kuwa Katiba za nchi zao zinakuwa na vipengele kwa ajili ya:
-Kuwa na tasnia ya habari ambayo ipo huru, salama na yenye kujitegemea ikijumuisha usalama wa wanahabari.
-Sheria nyingine zote ziheshimu Katiba za nchi zikiendana na vyombo na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu.
2. Wamiliki wa vyombo vya habari wafanye marekebisho ya miundo ambayo itazingatia yafuatayo;
- Uendeshaji bira- Ikiwa ni pamoja na masuala ya Ajira, Mishahara, Mikataba, Motisha na Marupurupu mengine ya kifedha.
- Viendeshwe kwa kufuata na kuheshimu miiko ya Kitaaluma.
-Kuhakikisha kuwa wanahabari wote wanakuwa na Bima.
-Vyumba vya habari viongeze uwekezaji katika mitandao ya kijamii pamoja na utoajji elimu kwa wanahabari kuhusu mitandao binafsi yaani Blogs.
3. Baraza la Habari lishirikiane na taasisi na vyama vya kitaaluma vya wanahabari ili kudumisha na kulinda ueledi na umoja katika tasnia ya habari.
4. Wanahabari waanzishe vyama vya wafanyakazi ili kuwezesha na kuongeza mapatano na makubaliano ya hiari sehemu za kazi.
5. Wamiliki wa vyombo vya habari walinde na kutetea usalama wa wanahabari na vyombo vyao kupitia
-Wamiliki wa vyombo vya habari kuweka na kuzingatia taratibu za usalama sehemu za kazi
-Wamiliki wa vyombo vya habari wahakikishe wanwapatia waandishi wa habari vifaa vya usalama au vya kujikingia na hatari na wawezeshe mafunzo juu ya taratibu za usalama.
-Kujumuisha mitaala ya mafunzo ya usalama na ulinzi katika taasisi zote za mafunzo ya uandishi wa habari.
- Wanahabari wao binafsi wachukue vipaumbele na tahadhari katika usalama wao binafsi.
6. Jumuiya ya Afrika Mashariki lizitake nchi wanachama wake ambao walitia sahihi itifaki ya Udhibiti wa Tovuti wajiondoe katika Mkataba huo ikiwa ni njia moja wapo ya kudumisha utawala bora na uwajibikaji.
7. Serikali za Afrika Mashariki zifanya juhudi katika kuwezesha uanzishwaji wa mfumo wa kisheria wa kuruhusu uendeshaji bora wa mitandao ya kijamii na wakati huo huo wakilinda uhuru wa wadhibiti ili kuboresha na kuendeleza uhuru wa mitandao ya kijamii katika eneo la Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment