Taifa
Stars imepoteza mechi ya ugenini baada ya kufungwa mabao 2-1. Mechi
hiyo ya kundi C ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la
Dunia mwakani nchini Brazil dhidi ya Morocco imechezwa leo (Juni 8 mwaka
huu) usiku kwenye uga wa Grand Stade de Marrakech, jijini Marrakech.
Licha
ya kufungwa, Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kumjaribu kipa wa Morocco,
Nadir Lamyaghri aliyeokoa shuti la mpira wa adhabu la Aggrey Morris
katika sekunde ya 40 tu tangu refa Daniel Frazier Bennett kutoka Afrika
Kusini apulize filimbi ya kuanzisha pambano hilo.
Refa
alitoa faulo hiyo baada ya mshambuliaji Thomas Ulimwengu kukwatuliwa na
Ahmed Kantari baada ya kumtambuka beki mwingine wa Simba hao wa milima
ya Atlas.
Stars
walicheza pungufu kwa dakika 58 baada ya Morris kutolewa nje kwa kadi
nyekundu kwa kumkwatua ndani ya eneo la hatari Abdelaziz Barrada huku
akiwa amebaki yeye na mshambuliaji huyo. Adhabu hiyo iliandamana na
penati ambayo Morocco waliitumia kupata bao la kuongoza dakika ya 37
mfungaji akiwa Abderazzak Hamed Allah.
Kabla,
Stars wanaodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager walitengeneza nafasi
nzuri ya kufunga dakika ya 25 baada ya Ulimwengu kufanikiwa kuwatoka
mabeki wawili wa Morocco na kuingia eneo la hatari lakini shuti lake
hafifu lilidakwa na kipa Lamyaghri.
Morocco
waliongeza bao lingine dakika ya 50 na Youssef El Arabi baada ya mabeki
wa Stars kujichanganya katika kudhibiti pasi ya mwisho ya wachezaji wa
timu hiyo, na mshambuliaji huyo kumfunga kirahisi kipa Juma Kaseja.
Kiungo
mshambuliaji Amri Kiemba aliifungia Stars bao maridadi dakika ya 61 kwa
mkwaju wa mbali uliomshinda kipa Lamyaghri. Kabla ya kuachia shuti
hilo, Kiemba aliwatoka wachezaji wa timu ya Morocco ambayo ndiyo imepeta
ushindi wake wa kwanza katika mechi hizo za mchujo za Kombe la Dunia.
Dakika
sita kabla ya filimbi ya mwisho Mbwana Samata angeweza kuisawazishia
Stars, lakini licha ya kuwatoka mabeki wawili wa Morocco baada ya
kupokea pasi ya John Bocco mpira aliopiga ulitoka nje.
Stars
ambayo bado inashika nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi
sita inaondoka hapa kesho (Juni 9 mwaka huu) mchana kwa ndege ya
EgyptAir kupitia Cairo, Misri na itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11 alifajiri (Juni 10 mwaka huu).
Katika
mechi hiyo Stars iliwakilishwa na; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari
Kapombe, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa/Nadir
Haroub, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu/Khamis Mcha/John Bocco, Amri
Kiemba na Mbwana Samata.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Marrakech, Morocco
+212 610120619
No comments:
Post a Comment