Sunday, July 21, 2013

Mashindano ya kusoma Quran tukufu kitaifa yamalizika



Msomaji wa Quran tukufu katika mashindano ya kitaifa, Seif Salim Said ambaye ni mremavu wa macho akisoma wakati wa fainali zake leo

Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya kitaifa ya kuhifadhi Quran tukufu yamemalizika leo, huku walemavu wa viungo wakiwa kivutio cha aina yake, kwa kuonyesha maajabu.
Walioshangiliwa na hata kuwatoa machozi watazamaji walikuwa ni Ummy Kuluthumu Swaleh Saidi kutoka Pemba, ambaye hakuwa na miguu wala mikono pamoja na  Seif Salim Said ambaye ni mlemavu wa kuona na kusikia, waliweza kusoma vizuri bila kubabaika huku wakiwapita hata wale waliokuwa na viungo kamili.
Mashindano hayo yalimalizika jana Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo yalihusisha washiriki 72 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
Walemavu hao pamoja na wengine sita, walizawadiwa fedha taslim  pamoja na fimbo za kuwawezesha kutembea.
Nafasi ya mshindi wa kwanza kwa wavulana ilikwenda kwa Abdul Hamid na msichana alikuwa Suria Ally Bakari ambao kwa pamoja walipewa  Bajaji na fedha taslim sh. 500,000.
Washindi wa mashindano hayo yaliyoandaliwa na Eshe Sururu Foundation, yaligawanywa katika makundi matano, kwa upande wanawake na wanaume, huku washindi  wengine wakiondoka na pikipiki, baiskeli, vyereheni na fedha taslim.
Katibu wa kamati ya maandalizi, Issah Ramadhan Mohamed alisema kuwa madhumuni ya kuandaa mashindano hayo ni kuibua ari kwa vijana wa kiislam waweze kusoma Quran Tukufu  kwa mustakabali wa maisha mema.
Alisema yalishirikisha wasichana 38 na wavulana 34 ambapo kila upande alitoka mshindi wa kwanza hadi wa tatu na yaligawanywa kwa ngazi tano ikiwemo kuhifadhi Juzuu 20,10, tano na tatu.

No comments:

Post a Comment