Thursday, August 22, 2013

Banyai atamba kuipa mafanikio Ashanti


Kocha mpya wa Ashanti United, Hassan Banyai (kulia)



ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Moro United, Hassan Banyai, ameteuliwa kuchukua mikoba ya Hassan Mubaraka 'Muba' wa Ashanti United baada ya kocha huyo kukosa sifa za kufundisha Ligi Kuu Bara, na ameapa kuendeleza makali ya timu hiyo.

Muba ambaye alijiwekea rekodi mpya baada ya kuipandisha timu hiyo kwa mara ya pili Ligi Kuu, ameshindwa kuendelea kuinoa timu hiyo baada ya kutotimiza vigezo vya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA).

Kwa mujibu wa taratibu za TAFCA, kocha anayepaswa kufundisha Ligi Kuu ni yule mwenye cheti kuanzia ngazi ya Kati (Intermidiate Course).

Akizungumza na Nyumba ya Michezo na Burudani, Katibu Mkuu wa Ashanti United, Abubakari Silas, alisema  baada ya TAFCA kutoa angalizo hilo wameona ni bora wakajipanga mapema ili kuepuka usumbufu watakaoupata baadaye

"Baada ya uongozi kushauriana kwa kina na kugundua kwamba kocha tuliyenaye hajakidhi viwango vya TAFCA licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kufundisha, ndio maana tukaamua kumchukua Hassan Banyai," alisema.

Alisema wanamuheshimu Muba na wataendelea kumthamini kwa kazi kubwa aliyoifanyia timu hiyo na wana imani hiyo ni changamoto kwake atakayoichukulia katika mtazamo mzuri zaidi wa kimaendeleo.

Mbali na hilo, Silas alisema pia wamekubaliana Rais wa timu hiyo wa sasa, Msafiri Mgoyi, aendelee kuwa katika nafasi hiyo akisaidiwa na Almasi Kasongo katika umakamu rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).

Akizungumzia zaidi timu yao iliyoko nchini Burundi kujiwinda na ligi kuu, alisema inaendelea vizuri na kwamba imecheza mechi moja na timu ya daraja la kwanza nchini na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Alisema bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wao ambaye pia ni mshauri wa benchi la ufundi, Said Maulid 'SMG' katika mchezo walioonesha kiwango kizuri na wanatarajia kurudi jijini Ijumaa.

Kwa upande wake, Banyai ametamba kuipa mafanikio timu hiyo na kuwaahidi mashabiki wa Ashanti kutumia uwezo wake wote kwa ajili ya timu hiyo.

No comments:

Post a Comment