Mlinda mlango wa Taifa Stars Juma Kaseja |
NAHODHA wa timu ya soka
ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Juma Kaseja amesema kwamba
amefanya mazungumzo tu na wakala wa klabu ya St. Eloi Lupopo ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini bado hajaingia Mkataba na klabu
hiyo ya Lubumbashi.
Akizungumza jana mchana,
Kaseja amesema kwamba mtu aliyejitambulisha kwake kama wakala wa Lupopo
alimfuata wakafanya mazungumzo na kufikia makubalino juu ya dau la
usajili, mshahara na mambo mengine ya msingi.
Hata hivyo, kipa huyo
namba moja Tanzania amesema kwamba baada ya mazungumzo hayo na
maafikiano, wakala huyo amepeleka majibu Lupopo ambao wakiafiki ndipo
masuala ya Mkataba yatafuatia.
“Nimezisikia
hizo habari, kwamba mimi tayari ni mchezaji wa Lupopo, hapana, si
kweli. Ni kwamba tumefanya mazungumzo tu na wakala wao na tumefikia
makubaliano, nasubiri hadi nisaini Mkataba ndipo nitajihesabu tayari ni
mchezaji wa Lupopo,”alisema Kaseja.
Baada ya kuitumikia Simba
SC tangu mwaka 2003, Kaseja hakuongezewa Mkataba klabu hiyo mwishoni mwa
msimu naye ameamua kwenda kuanza maisha mapya sehemu nyingine.
Pamoja na Simba SC kutomuongezea Mkataba Kaseja, ameendelea kuwa kipa chaguo la kwanza timu ya taifa mbele ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen.
Iwapo Kaseja atafanikiwa
kuingia Mkataba na Lupopo atakwenda kuwa mpinzani mkuu wa wachezaji
wenzake wa Taifa Stars, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea
Tout Puissant Mazembe ya Lubumbashi.
Kaseja alicheza pamoja na
Samatta na kiungo Mganda wa Mazembe, Patrick Ochan katika klabu ya Simba
mwaka 2010 kabla ya 2011 wachezaji hao kuuzwa DRC.
No comments:
Post a Comment