Friday, August 23, 2013

TMAA YAWANASA WATOROSHAJI WA MADINI


  Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA Bruno Mteta, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu madini yaliyokamatwa. wa pili kushoto ni Ofisa habari wa TMAA, Mhandisi, Yisambi Shiwa na kulia ni Mkurugenzi wa Uthamini Madini na Huduma za Maabara, Mhandisi, Rwekaza Dominic.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA Bruno Mteta, akifafanua jambo. Kushoto ni Ofisa habari wa TMAA, Mhandisi, Yisambi Shiwa.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA Bruno Mteta, akionesha sehemu ya madini yaliyokamatwa.
Sasa tumeanza kazi.
Haya ni baadhi ya madini yaliyokamatwa na TMAA.


Na Irene Mark

WAKALA wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) umekamata shehena ya madini yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 13 katika kipindi cha miezi 10 iliyokuwa ikitoroshwa nchini kinyume cha utaratibu.

Madini hayo yalikamatwa kwenye viwanja mbalimbali vya ndege hapa nchini ambapo wakaguzi wa TMAA kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji, Usalama wa Taifa, watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Jeshi la Polisi na wafanyakazi wa viwanja vya ndege (TAA).

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za wakala huyo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA Bruno Mteta alisema madini hayo yalikamatwa kati ya Septemba mwaka 2012 na Julai mwaka huu katika matukio 23 tofauti.

Alisema kwa mwezi huu tayari wakala huyo umewakamata raia wawili wa kigeni wakiwa na shehena ya madini wakitaka kutoroka nayo huku akisisitiza kwamba watapandishwa kizimbani wakati wowote.

“Agosti 20 mwaka huu tumewakamata raia wawili wa kigeni mmoja alikuwa anasafiri amekamatiwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) akiwa na madini ya vito yenye thamani ya sh milioni 25.32.

“…Wa pili amekamatwa akiwa kwenye makazi yake Jangwani Beach hapa jijini kwa kweli thamani ya madini ya mtuhumiwa huyu hayakutambukuka,” alisema na kuongeza kuwa serikali imeyataifisha madini hayo.

Kwa mujibu wa Mteta wafanyabiashara wa kigeni na wazawa wanaruhusiwa kusafirisha madini hayo kwa kuzingatia utaratibu ili serikali ipate mgao wake huku akisisitiza kwamba serikali inategemea mapato ya madini kujiendesha.

Awali mkurugenzi huyo alisema tangu mwaka 2009 hadi mwishoni mwa mwaka jana serikali imepokea sh bilioni 317.74 ambazo ni mrabaha uliolipwa na kampuni 10 kubwa za madini hapa nchni. 
Alisema hivi sasa wizi wa madini kwenye migodi mikubwa haupo kutokana na uwepo wa watumishi wa TMAA wanaotoa ripoti ya uzalishaji kila siku na kwamba wafanyabiashara wa madini wanaoongoza kwa kukwepa kodi ni wazawa.

Mteta alieleza changamoto zinazoukabiliwa wakala huyo kuwa ni kushindwa kuifikia mipaka yote inayounganisha nchi jirani (njia za panya) ambazo hutumika na wafanyabiashara wengi kutorosha madini hayo.

Alisema watoroshaji wengi wa madini hayo ni wageni kutoka nchi mbalimbali ambao wanauziwa madini na watanzania na kufafanua kwamba kati ya matukio 23 watanzania wawili.

Mkurugenzi huyo alisema tayari kesi tatu kati ya 23 zimesikilizwa na kutolewa hukumu na kutoa mfano wa kesi ya mgeni aliyekamatwa na madini yenye thamani ya zaidi ya Dola 6,200 za Marekani alitozwa faini ya sh milioni 1.5 na madini yake kutaifishwa na serikali.

No comments:

Post a Comment