Friday, October 11, 2013

Hotuba za marehemu Baba wa Taifa sasa kupatikana kiganjani


 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiki akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa huduma ya kupata hotuba za Marehemu baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika kwenye hotel ya Double Tree jana. Ili kuweza kupata hotuba za maneno na picha za video unatakiwa kutuma neno Hotuba kwenda namba 15678, pia unaweza kupata huduma hiyo kwa kutumiawww.simu.tv/nyerere mobile tv. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Push Media Mobile Freddie Manento
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Push Media Mobile, Freddie Manento  (katikati) akifafanua jambo kuhusiana na mpango wa kumuenzi marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  kupata hotuba zake mbali mbali kwa njia ya simu ya mkononi. Kushoto ni msaidizi maalum wa mkurugenzi mtendaji wa Taasisi mwalimu Nyerere, Gallus Abedi na kulia ni Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Push Media Mobile, Freddie Manento (kushoto) na Mkurugenzi wa Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku wakibadilisha mkataba mara baada ya kusainiwa katika  hafla ya uzinduzi wa huduma ya kupata hotuba za Marehemu baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika kwenye hotel ya Double Tree. Huduma hiyo inamwezesha mwananchi kupata hotuba mbali mbali mbali za marehemu Baba wa Taifa kwa kutuma neno Hotuba kwenda namba 15678. Pia unaweza kupata huduma hiyo kwa kutumia www.simu.tv/nyerere mobile tv.
Wafanyakazi wa kampuni ya Push Media Mobile na Taasisi ya Mwalimu Nyerere wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua huduma ya kumwezesha mwananchi kupata hotuba mbali mbali mbali za marehemu Baba wa Taifa kwa kutuma neno Hotuba kwenda namba 15678. Pia unaweza kupata huduma hiyo kwa kutumiawww.simu.tv/nyerere mobile tv.
======  ======= ========
WATANZANIA watapata fursa ya kuangalia na kupata hotuba za marehemu Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere kupitia mpango ulioanzishwa na taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya Push Mobile Media.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Butiku alisema  kuwa wameamua kuanzisha mpango  huo ili kuwawezesha watanzania, waafrika na dunia kwa ujumla kujua kazi alizozifanya marehemu Baba wa Taifa kwa jamii.
Butiku Alifafanua kuwa ili kuweza kupata hotuba hizo kupitia simu ya mkononi unatakiwakutuma neno Hotuba kwenda namba 15678 . Vile vile unaweza kupata picha nyingi zaidi kwa kuingia www.simu.tv/nyereremobile tv.
Alisema kuwa mpango huo upo kwa njia ya CD na DVD ambazo watanzania wengi wameanza kuzichangamkia kupata nakala.
“Huu ni mpango maalum wa kuhakikisha kumbukumbu za marehemu baba wa Taifa zinapatikana kiganjani na muda wowote, tumeingia makubaliano maalum  na kampuni ya Push Media Mobile ili kuendeleza juhudi hizi za kuenzi enzi zake,” alisema Butiku.
Alisema kuwa marehemu Mwalimu amefanya kazi kubwa za kuelimisha kwa kutunga vitabu mbali mbali ambavyo vingi vimekuwa vikutumika kusaidia mambo mbali mbali ya kisiasa na uchumi.
“Nakumbuka alisema kuwa mawazo haya yapo kwenye vitabu na kanda mbali mbali, yatumike katika kuchangia maendeleo ya  binadamu, alikuwa mwangalifu sana kwani yamezingatia hali halisi ya jana na leo, natoa ushauri kwa watanzania kutumia mpango huu ili kusaidia taifa,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Push Mobile Media Freddie Manento alisema kuwa wameingia makubaliano na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na lengo kubwa ni kurahisisha kupatikana busara za Mwalimu kwa watanzania wote, ikiwa pamoja na vizazi vya sasa.
Manento alisema kuwa huduma hii moja ya njia ya kuendelea kumkumbuka Marehemu Baba wa Taifa ambaye pia ni muasisi wa Taifa hili.
Alisema kuwa sababu nyingine ya kuanzisha huduma hiyo ni kuwakumbusha Watanzania, Waafrika  na dunia kwa ujumla busara zake na hasa kwa njia ya hotuba zake ambazo si za kawaida kwani bado zinaendelea kuzungumzia mambo mbali mbali yanayotokea sasa.
Aliongeza kuwa mpango huo pia utaendeleza njia nyingine za kuenzi heshima ya marehemu Baba wa Taifa katika mchango wake wa kulikomboa taifa hili na mpiganaji wa haki za binadamu duniani.
Alisema kuwa hakuna asiyejua kuwa marehemu Baba wa Taifa ni mkombozi wa haki za wanyonge na alikuwa mstari wa mbele katika kupigiania Uhuru wa Tanzania na mataifa mengine katika bara la Afrika.
Alisema kuwa mchango wake hauwezi kusaulika na vizazi vilivyopo wakati wa uhai wake na vizazi vipya vitakuwa na hamu kubwa ya kupata falsafa zake kupitia hotuba mbali mbali ambazo zimekuwa zikitumika katika nyanja nyingi hapa nchini.
“Ili kurahisisha upatikanaji wa hotuba hizo, tumeamua kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation na kuanzia sasa, unatweza kupata hotuba yake kwa njia ya televisheni na kwa njia ya meseji kwa kupitia simu ya mkononi  na kuendelea kumuenzi marehemu Baba wa Taifa,” aliongeza.
Alisema kuwa huduma hii ni ya mara ya kwanza kutokea hapa nchini ambapo Watanzania watapata fursa ya kuona na kusoma hotuba ya marehemu baba wa Taifa kwa njia ya mtandao wa simu ya mkononi.

No comments:

Post a Comment