Katibu
Mkuu wa Taswa Tanzania, Amir Mhando (katikati) akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam, leo mchana kuhusu sherehe za utoaji wa
tuzo kwa wanamichezo bora wa mwaka 2012, zinazotarajia kufanyika hivi
karibuni. Kushoto ni Mwenyekiti wa tuzo hizo, Haji Manara (kulia) ni
mjumbe wa tuzo hizo, Salum Jaba.
******************************************
CHAMA cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA), kimekuwa na utaratibu wa kila mwaka kutoa
tuzo kwa wanamichezo wanaofanya vizuri na sherehe za utoaji wa tuzo hizo
zimekuwa zikifanyika kati ya miezi ya Mei na Juni.
Hata
hivyo mwaka huu tuzo hizo zimechelewa kufanyika kutokana na sababu
mbalimbali, ambazo zipo nje ya uwezo wa Kamati ya Tuzo, Kamati ya
Utendaji ya TASWA, wanachama wa TASWA, wanamichezo husika na wandishi wa
habari za michezo kwa ujumla wao.
Ndugu zangu ninyi ni mashahidi wa tuzo za miaka miwili iliyopita, zilivyofana na zikabaki kupigiwa mfano kwa ubora wake.
Lakini
mwaka huu, mambo kidogo yalikuwa magumu kutokana na kampuni ambayo
sitaitaja jina, ambayo awali ilituhakikishia ingedhamini kwa asilimia
100 lakini ilipata matatizo ya kiuchumi wiki tatu kabla ya tarehe
tuliyokuwa tumepanga kufanya tuzo, hivyo wakatuomba tusogeze mbele
huenda mambo yangeimarika.
Kuanzia
hapo kila mara wakawa wanatuhakikishia mambo yatakuwa mazuri, lakini
mwezi Agosti mwishoni wakatupa taarifa rasmi kuwa hawatamudu kudhamini
tuzo zetu, hali ambayo ilituchanganya kwa kiasi kikubwa kwani ingekuwa
vigumu sana kupata wadhamini wa ghafla kwa wakati huo.
Hata
hivyo kutokana na heshima ambayo TASWA imejijengea na kuaminika mbele
ya jamii kwa kushirikiana na Kamati ya Tuzo, tukaanza mazungumzo na
kampuni mbalimbali na tayari tumepata kampuni mbili za kutusaidia, huku
tukiendelea na juhudi zetu za kupata wadhamini wa kutosha kulingana na
bajeti yetu.
Leo
ninayo furaha kuwatangazia kuwa Desemba 20 mwaka huu, tutafanya Tuzo ya
Wanamichezo Bora wa mwaka 2012 katika ukumbi ambao tutautangaza hivi
karibuni na maandalizi yamefikia hatua nzuri sana.
Tumefanya
vikao kadhaa cha mwisho kikiwa jana kati ya Kamati ya Utendaji ya TASWA
na Kamati ya Tuzo, tumetafakari athari za kuchelewa kufanya na zile za
kuacha kufanya, tukajiridhisha ni bora tufanye ingawa tumechelewa,
lakini lazima tuwaenzi wanamichezo waliofanya vizuri mwaka uliopita.
Tunaomba
radhi wanamichezo wanaowania tuzo hizo, vyama mbalimbali vya michezo na
wote ambao kwa namna moja au nyingine kuchelewa kwetu kuliwakwaza,
lakini hatukuwa na jinsi yote ni katika kuhakikisha tuzo zetu zinakuwa
bora kama miaka iliyopita.
Tayari
majina ya awali ya wanaowania tuzo kwa michezo mbalimbali
tulishayatangaza, ni jukumu sasa la Kamati ya Tuzo kuendelea na mchakato
ili kuhakikisha zinakuwa nzuri zaidi.
Ahsanteni
Haji Manara
Mwenyekiti Kamati ya Tuzo
3/10/2013
No comments:
Post a Comment