Thursday, November 7, 2013

NEWS ALERT: ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege APANDISHWA KIZIMBANI LEO


Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekerege (pichani) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka mawili ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa asilimia 50 ya punguzo la ada ya utawala kwa Kampuni mbili na kulisababishia shirika hilo hasara ya Dola 42,543 za Kimarekani.

Kampuni hizo ni, Jaffar Mohamed Ali Garage na Quality Motors za jijini Dar es Salaam.  Ekerege alifikishwa mahakamani hapo Jumatano mchana kimya kimya na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Ausustina Mmbando.

 Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Machuya alidai kwamba kati ya Machi 28 mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, katika ofisi za TBS iliyopo wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu Ekerege alitumia madaraka yake vibaya.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa punguzo la asilimia 50 ya ada ya utawala kwa kampuni hizo bila idhini ya baraza la utendaji la TBS kinyume cha sheria namba 2 kifungu kidogo cha (3) ya TBS ya mwaka 2005. 

Ilidaiwa kuwa kitendo hicho kiliziongezea kampuni hizo faida ya Dola 42,543 za Kimarekani sawa na (kwa wakati huo) Sh. Milioni 68,068,800. 
Upande huo wa Jamhuri ulidaiwa shitaka la pili, katika tarehe na mahali pa tukio la kwanza, mshtakiwa alilisababishia shirika kupata hasara ya fedha hizo. 

Mshtakiwa alikana mashitaka yote mawili na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na haukuwa pingamizi la kutoa dhamana dhidi ya mshtakiwa. 

Hakimu Mmbando alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka kwenye taasisi za kuaminika watakaosaini hati ya Sh. Milioni 35 kila mmoja. 

Mshtakiwa alitimiza masharti hayo ya dhamana na yuko nje hadi Desemba 12, mwaka huu atakaposomewa maelezo ya awali.Chanzo Michuzi Blog

No comments:

Post a Comment