Saturday, December 14, 2013

HALI TETE BARAZA LA MAWAZIRI



mawaziri+clip (1)Rais Kikwete akiendesha kikao cha baraza la Mawaziri siku za hivi karibuni. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali. Picha na Maktaba.
………………………………………………………………
Dodoma. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, jana alilithibitishia gazeti dada la Mwananchi, The Citizen juu ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu (CC), lakini hakuwa tayari kuingia kwa undani kuhusu ajenda.
Hata hivyo, habari za ndani zilieleza kwamba miongoni mwa ajenda kuu za CC ni kuwahoji mawaziri wanaolalamikiwa na wananchi, kwamba wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Wakiwa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Nape aliwatupia lawama mawaziri wakati akielezea changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Mawaziri waliotajwa mzigo ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima, kwamba wameshindwa kazi na alipendekeza wang’olewe.
Hata hivyo, gazeti hili jana lilishuhudia mawaziri kadhaa wakifika na kuingia kwenye mkutano wa CC, taarifa zingine zilisema mawaziri waliofika kwenye kikao hicho walihojiwa na wajumbe wa CC.
Kuhojiwa na CC
Mawaziri waliohojiwa na CC hadi kufikia saa 8:00 mchana jana walitajwa kuwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza. Mkuya ndiye ambaye kwa sasa anaisimamia Wizara Fedha kutokana na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kulazwa nchini Afrika Kusini akisumbuliwa na maradhi ambayo hayajatajwa.
Waandishi wa gazeti hili jana waliwashuhudia takriban mawaziri 10 wakiingia katika ofisi za makao makuu ya CCM, Dodoma, maarufu White House, huku baadhi wakiwa si wajumbe wa CC.
Habari zilizotufikia jioni ziliwataja wengine kuwa ni Dk David Mathayo David (Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Hawa Ghasia (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), Dk Kawambwa, Celina Kombani (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma).
Dk Kawambwa wakati akitoka kwenye kikao cha CC aliulizwa na waandishi wa habari kilichotokea na yeye alijibu kwa kifupi; “Mawaziri mizigo ndiyo tunatoka.”
Mawaziri ambao si wajumbe wa CC ni Mkuya, Chiza, Dk Kawambwa, Hawa Ghasia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora, George Mkuchika ambaye naye taarifa zilidai alihojiwa.
Tayari Bunge limepitisha azimio la kumtaka Ghasia pamoja na naibu mawaziri wake wawili, Aggrey Mwanry na Majaliwa Kassim Majaliwa, kupima na kutafakari kama bado wanatosha kusimamia wizara hiyo.
Kiini cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kubainisha kuwapo wizi, ubadhirifu na mtandao wa ufisadi ndani ya Tamisemi, Halmashauri na Hazina.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye baadhi ya wabunge wamemtaja kama waziri mzigo namba moja, amesema yuko tayari kuachia ngazi kama Rais ataamua kumwondoa katika wadhifa huo.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la papo kwa hapo kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Ahmed (Cuf) aliyetaka aeleze anajisikiaje kuitwa mzigo namba moja.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia wizara 20, hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa sababu ya wizara moja ama mbili kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki.
Alisema kama Rais atamwona ameshindwa kuwajibika yuko tayari kuachia ngazi na endapo Rais hatafanya hivyo na wabunge bado wakaona ipo haja hiyo, wampigie kura ya kutokuwa na imani naye.
Kauli ya CCM
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, alisema kuwa mawaziri hao wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.
Alisema kuwa Waziri Chiza na Malima wamebaki wakifunga tai na kuvaa suti mjini wakati wakulima wa Ruvuma na mikoa mingine ya Tanzania wakiteseka.
Nape alisema Waziri Kawambwa naye anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kuingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya kutengeneza barabara ya Namtumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga na matokeo yake amefukuzwa kazi.
Dk Kawambwa ametupiwa lawama hizo kutokana na kuipa kazi kampuni hiyo wakati akiwa Waziri wa Miundombinu pamoja na kushindwa kusimamia elimu.
“Katibu Mkuu (Kinana), nilimuuliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Chiza na Malima wamefika lini kusikiliza matatizo ya wakulima wa tumbaku, korosho na mahindi, alinijibu hakumbuki kama wamefika mkoani hapa. Nikafuatilia na kubaini si yeye tu hata Waziri aliyetangulia Profesa Jumanne Maghembe naye hakuwahi kufika. Najiuliza sababu nini, hakuna majibu,” alisema Nape.
Alisema anasikitishwa na kitendo cha mawaziri hao waliopewa dhamana kushindwa kutambua wajibu wao na kwamba umefika wakati wa kuhojiwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM, ili wachukuliwe hatua kwani bila kufanya hivyo aibu itarudi kwa chama chake.
Wabunge wajitosa
Kikao hicho cha CC kinafanyika huku kikiwa na taarifa kwamba wabunge wa chama hicho tawala wameanza kukusanya saini za wabunge, ili kushinikiza kuitishwa kwa kikao cha wabunge hao au Party Cocas.
Uchunguzi wa gazeti hili, uliofanywa kwa siku kadhaa mjini hapa, umebaini kuwa wabunge wa CCM zaidi ya 160 wametia saini katika fomu hiyo wakiwamo mawaziri zaidi ya 10.
Chanzo kimoja cha kuaminika kilisema kuwa fomu hiyo iliwasilishwa katika ofisi ya katibu wa wabunge wa CCM, ikiambatana na barua inayotaka kuitishwa kwa kikao kitakachowakutanisha.
“Tuliwaomba waitishe kikao cha wabunge wa CCM ili mawaziri ambao tunawaona hawatimizi majukumu yao kikamilifu waweze kuhojiwa lakini wakawa wanasuasua,”kilisema chanzo hicho.
“Lakini mmoja wetu akasema kwa kuwa wamepiga chenga ya kukiitisha basi kuna nafasi ya kikanuni ya kukusanya saini za wabunge zaidi ya nusu kushinikiza kuitishwa kwa kikao,”alisema mbunge huyo.
Taarifa ya ziada na Habel Chidawali
Mbunge mwingine wa CCM alisema katika kikao hicho wabunge walitaka kukutanishwa kwa pamoja kati yao, mawaziri wanaoonekana kuwa mzigo na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
“Kikao hicho tulitaka kiwe Desemba 12 mwaka huu ili tuanze kuwahoji mawaziri kabla ya CC lakini Mwenyekiti (Mizengo Pinda), amekuwa akipiga danadana hadi leo (jana) inapokutana”alisema.
Habari zaidi zilisema baadhi ya wabunge wa CCM walikutana faragha na Kinana juzi jioni na kumtahadharisha kama mawaziri hao wasipowajibishwa, CCM kitakuwa na wakati mgumu.
Vuguvugu linaloendelea hivi sasa ndani ya wabunge wa CCM, liliwahi kujitokeza Bunge la Aprili mwaka jana na kumlazimisha Rais Kikwete kupangua Baraza lake Mawaziri Mei 4,2012.
Kung’olewa kwa mawaziri sita waliokuwa wakishinikizwa na wabunge wajiuzulu kulitokana na taarifa za kamati za kudumu za bunge na za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika baraza lake hilo jipya, Rais aliwatosa mawaziri waliokuwa wakishinikizwa kujiuzulu akiwemo Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami.
Wengine waliotoswa kwa shinikizo hilo lililoungwa mkono na kambi ya upinzani ni wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, wa Nishati na Madini, William Ngeleja na wa Uchukuzi, Omar Nundu.
Pia Naibu Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk Athuman Mfutakamba naye alitoswa sambamba na Waziri wa Afya, Dk Haji Hussein Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya.
 CHANZO: MWANANCH

No comments:

Post a Comment