* Sikinde yajichimbia mjini Bagamoyo
* Msondo washindwa kutaja kambi ilipo
Baadhi ya wanamuziki wa Sikinde |
Baadhi ya waimbaji wa Msondo Ngoma |
HOMA
ya pambano la watani wa jadi katika muziki wa dansi nchini kati ya Mlimani Park
'Wana Sikinde' na Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' litakalofanyika siku ya
Krismasi imeanza kupanda kwa bendi hizo kujificha kambini na huku wakipigana
vijembe.
Bendi
hizo kongwe nchini zinatarajiwa kuonyeshana kazi katika onyesho litakalofanyika
kwenye viwanja wa TCC Club Chang'ombe, Temeke Dar es Salaam katika kunogesha
sikukuu hiyo ya Krismasi.
Katika
kuonyesha wamelipania pambano hilo bendi ya Sikinde tayari imeiendea Msondo
wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kuweka kambi yao na wamewatahadharisha
'mahasimu' wao hao wasije wakatoa visingizio baada ya kugaragazwa kwenye
onyesho hilo.
"Sisi
tumeamua kuweka kambi yetu mjini Bagamoyo ambako tutatua viwanja vya TCC
kutokea huko ili kuisambaratisha Msondo, na tunataka wajipange sawasawa ili
wasije wakatoa visingizio tena kwa maana kama vyombo vipya bendi zote imepewa
na Konyagi," Katibu wa Sikinde, Hamis Milambo alisema.
Milambo
alisema mashabiki wa dansi wajitokeze kwa wingi kushuhudia namna gani
wanavyowachachafya wapinzani wao hao, ikizingatiwa hawajakutana kwa muda tangu
mwaka jana.
Upande
wa Msondo kupitia Meneja wao, Said Kibiriti, alisema hawana haja ya kutaja
mahali kambi yao ilipo isipokuwa wamejiandaa kuwatoa nishai wapinzani wao siku
ya onyesho hilo litakaloanza saa nane mchana.
"Sisi
hatuna mchecheto wowote na mpambano huo, tunaendelea kujifua kimya kimya mahali
ambapo siwezi kupataja kwa sasa," alisema Kibiriti.
Naye
muimbaji anayekuja juu wa bendi hiyo ya Msondo alitokea Sikinde, Athuman Kambi,
alisema amejipanga kuonyesha umahiri wake katika mpambano huo baada ya kufanya
hivyo wakati akiwa Sikinde dhidi ya Msondo kwenye ukumbi wa Diamond na
kuwawehusha mashabiki wa muziki wa dansi nchini.
"Najua
watu watataka kuona nafanya kitu gani dhidi ya bendi yangu ya zamani
iliyonitangaza vyema, wasiwe na hofu waje Desemba 25 waone nini nitakachofanya
TCC Club Chang'ombe," alisema Kambi.
Mpambano
huo wa Sikinde na Msondo umeandaliwa na kampuni ya Bob Entertainment na Keen
Arts chini ya udhamini wa Konyagi, gazeti la NIPASHE, Integrated
Communications, CXC Africa na Salute5.
No comments:
Post a Comment