Nahodha wa timu ya Taifa ya wanawake, ‘Twiga stars’, Sophia Mwasikili akiwatambulisha wachezaji wenzake (hawapo kwenye picha) kwenye kongamano la wanawake wa Afrika viongozi wa michezo |
WASHIRIKI wa kongamano la wanawake viongozi wa Afrika
linalofanyika nchini leo watafanya bonanza la michezo yote katika Uwanja wa
Taifa Dar es Salaam.
Akizungumza na Habari Leo, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo wa
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ambaye ndiye mwandaaji wa
kongamano hilo Juliana Yasoda alisema
kuwa watafanya bonanza hilo ambalo litajumuisha michezo yote katika Uwanja wa
Taifa kuanzia saa 3:00 asubuhi.
“Kesho (leo) tutafanya bonanza ambalo litahusisha michezo
yote kwani hapa kuna viongozi na wanamichezo wa michezo yote na baadae timu za
Taifa ya Twiga na ile U-20 watacheza mchezo wa kirafiki”, alisema Juliana.
Michezo ambayo itachezwa ni soka, riadha, kikapu, mikono,
wavu, magongo, kurusha tufe na kisahani pamoja na kuvuta kamba.
Pia alisema kongamano hilo limesaidia kutoa mwanga na dira
kwenye michezo miongoni mwa washiriki kutokana na kila mmoja kuelezea uzoefu
wake katika michezo ukilinganisha na sera za nchi anayotoka.
Awali juzi wakati akifungua kongamano hilo Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mh. Amos Makala aliwataka washiriki hao
kupigania michezo katika nchi wanazotoka
kwani wanawake ni chachu ya mafanikio kwenye michezo mbalimbali hasa
wakipewa elimu ya maendeleo ya michezo.
Kongamano hilo lilikuwa la siku mbili na lilishirikisha
viongozi wanawake toka nchi za Msumbiji, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Zambia
na Ghana pamoja na wageni wengine toka Finland na
Marekani
No comments:
Post a Comment