Tuesday, January 14, 2014

Bonzo Kwembe kupakua nne za albamu binafsi


MCHARAZAJI gitaa maarufu nchini aliyewahi kuzipigia bendi mbalimbali ndani na nje ya nchi, Ismail Kwembe 'Bonzo Kwembe' anayemiliki bendi binafsi iitwayo 'The Bokwe Tunes Band' anajiandaa kuingia studio kurekodi albamu yake ya kwanza tangu ajitegemee (solo artist).
Bonzo aliiambia MICHARAZO kuwa, albamu hiyo itakayokuwa na nyimbo nne itapigwa katika miondoko tofauti ikiwamo Zouk na itawashirikisha wasanii kadhaa nyota na chipukizi nchini.
Mwanamuziki huyo alisema kwa kuanza ataanza kurekodi wimbo uitwao 'Mapenzi ya Mbali' atakaoimba na mwanamuziki mmoja mkongwe (jina hataki liwe hadharani kwa sasa) na Said Kaunga, chipukizi wa dansi na kipa wa zamani wa Toto Africans.
"Nitaanza na Mapenzi ya Mbali nitakayoimba na wanamuziki Said Kaunga niliye naye katika bendi yangu na mkongwe mmoja, kisha utafuata nyingine zilizosalia," alisema Bonzo.
Bonzo ambaye mbali na kupiga gitaa pia ni mtunzi na muimbaji kwa sasa, alizitaja nyimbo nyingine zitakazokuwa katika albamu hiyo ni pamoja na 'Shida za Dunia', 'Janga la Ukimwi',  na 'Upendo wa Moyo'.
Kuhusu bendi yake, Bonzo alisema inaendelea na maonyesho yake kwenye mahoteli na katika harusi kwa mialiko maalum wakiwa wakijikita kupiga na kuimba nyimbo za 'kukopi' za wasanii na makundi mbalimbali ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment