Friday, January 24, 2014

MJUE KWA UNDANI BONDIA AMIR KHAN




Amir Khan:

LEO katika safu hii ya maisha ya wenzetu tutakuwa tukiangazia maisha ya mwanamasumbwi, Amir Abdul Khan ambaye amepata kupendwa na kuwashika mashabiki wengi wa mchezo huo kutokana na umahiri, uwezo na mbwembwe anazokuwa anazifanya pindi  anapokuwa ulingoni.
Mbabe Khan ambaye ni raia wa Uingereza alikuwa bingwa wa dunia wa uzito wa WBA, WBA (Super) ikiwa ni pamoja na IBF, hivi sasa ameonesha nia ya kutaka kupambana na mbabe asiyepigika Floyd Mayweather Jr.
Zipo kila dalili zinazoashiria kwamba wawili hawa watachapana kutokana na kauli ambayo imewahi kutolewa na Mayweather Jr mwaka jana baada ya kumchapa Saul ‘Canelo’ Alvarez alisema kuwa anatarajia hadi kufikia Septemba mwakani awe amecheza mapambano manne na ya kwanza kuanza nayo ni mawili ambayo miongoni mwao yatakuwa kati yake na Amir Khan au bondia wa Argentina Marcos Maidana.

USICHOKIJUA
Ingawa watu wengi hufikiria kwamba Khan ni raia wa nchi za Asia lakini kijana huyo amezaliwa na kukulia Bolton, England, na wazazi wenye asili ya kipakistan wanaotokea katika jamii ya Punjab.
Khan ni muumini wa dini ya kiislam, na amekuwa akisaidia katika kuiwezesha tuzo inayotolewa na waislama wa nchini humo inayokwenda kwa jina la ‘Muslim Writers Awards’.
han anatoka katika familia yenye watoto wanne ambako ana dada wawili na kaka mmoja, Haroon ‘Harry’ Khan, mbabe asiyepigika.
Amir Khan ni mdogo wa mbabe na mshindi wa medali ya Olympic ya Uingereza, mshindi wa medali ya fedha ya olimpiki ya mwaka 2004 wakati akiwa na miaka  17.
Khan ana historia ya kukamata ubingwa wa dunia wa WBA akiwa na umri mdogo kuliko mwingireza mwingine wakati huo aliuchukua akiwa na miaka 22.
Ukiachilia ngumi ni mpenzi wa mchezo wa Kriketi, mpira wa kikapu na soka akiwa shabiki wa klabu ya Bolton Wanderers.
Mwaka 2012, alikuwa katika picha ya pamoja katika akaunti yake ya Twitter ikimuonesha akiwa na wachezaji wa Manchester United, Rio Ferdinand, Alex Buttner, Michael Carrick na David De Gea.
Lakini pamoja na kuonekana akiwa na nyopta hao huku akiwa amevaa jezi ya klabu hiyo lakini Khan alisema kuwa 'pamoja na kufanya hivyo lakini mimi bado ni shabiki wa klabu ya Bolton kwa njia yoyote.'




MSAADA WA KIJAMII
Khan amekuwa mtoaji mzuri wa misaada kwa watu wenye mahitaji kwa mfano mwaka 2004 alitoa msaada wa Euro milioni 1 kwa familia za wahindi waliokumbwa na tetemeko la Tsunami nchini India.
Katika mwaka huo alikwenda nchini Pakistan na kutoa vyakula katika kambi za watu waliokuwa wameathiriwa na tetemeko la Kashmir.[
Desemba 2013, Khan aliongoza harambee ya kuchangia Umoja wa waislam kutoka Ufilipino kwa ajili ya kutoa msaada wa waathirika wa tetemeko la Typhoon Haiyan na walikusanya kiasi cha Euro 83,400.
JINAI
Oktoba 23, 2007 Khan alitiwa mbaroni kwa kuendesha kwa kasi na alifikishwa katika mahakama ya Bolton kujibu shtaka lake ambako alifungiwa kuendesha gari kwa muda wa miezi sita ikiwamo na kupigwa faini ya euro 1000.
Mwaka 2006 aliwahi kupigwa faini ya Euro 40,000 kwa kosa la kuendesha kwa kasi.
Januari 7, 2008 Khan alipigwa faini ya Euro 1000 na kufungiwa kuendesha gari kwa siku 42.
Kama ilivyokawaida mwenye tabia yake hawezi kuacha Julai 12, 2009 Khan alijikuta akipata ajali ingawa hakufikishwa katika vyombo vya sheria.
 
MAHUSIANO
Januari 29, 2012 Khan alifunga ndoa na mwanamke wa Marekani mwenye asili ya Pakistani, Faryal Makhdoom katika harusi ya kifahari iliyohudhuriwa na ndugu na marafiki waliofikia 1000 akiwamo bondia Ricky Hatton.
Wawili hawa walifanya sherehe ya harusi yao Mei 31, 2013 huko Waldorf Astoria jijini New York, Marekani.
Baada ya kumalizika kwa sherehe hiyo ya kifahari wawili hawa walichukua ndege na kwenda nyumbani kwao na Khan huko Bolton kwa ajili ya kufanya sherehe nyingine ya kimila iliyofanyika Manchester na kuhudhuriwa na wageni 4,000.
FEDHA
Mbabe Amir Khan  anamiliki utajiri unaofikia dola milioni 23 (sawa na shilingi bil 36.8).

MAKAZI
Mbabe Amir Khan ana mjengo wa maana ambao hajaweka thamani yake lakini pia anamiliki gari mbalimbali ikiwamo Range Rovers, Bentley Continental, New Mercedes CLS63, Audi R8, Lamborghini Murcielago na Can-Am Spyder.

WASIFU
JINA: Amir Iqbal Khan ‘King’
KIMO: Futi 5 na inchi 9
UMRI: 27
Mapambano ya kucheza: 31
Ushindi: 28
KO:     20
Poteza:    3
Sare: 0
Makala hii imeandaliwa na Shabani Matutu.

No comments:

Post a Comment