Saturday, January 4, 2014

MKWASA, PONDAMALI, WATAMBULISHWA RASMI KWA WACHEZAJI KUANZA KUINOA YANGA


 

Uongozi wa Young Africans SC umepata warithi wa nafasi tatu za benchi la ufundi (Charles Boniface Mkwasa, Juma Pondamali na Dr. Suphian Juma), huku wakiendelea na mchakato kumpata kocha mkuu ambaye atachukua nafasi ya mholanzi Ernie Brandts aliyesitishiwa mkataba wake mwishoni mwa mwaka 2013.

Charles Boniface Mkwasa 'Master' aliyekua kocha mkuu wa timu ya Ruvu Shooting katika mzunguko wa kwanza anachukua nafasi ya aliyekua kocha msaidizi Fred Felix "Minziro" ambaye muda wake umemalizika mwishoni mwa mwaka 2013.

Mkwasa ambaye aliichezea Young Africans miaka ya 80's kwa kiwango cha hali juu pia alishawahi kuwa Kocha Mkuu/Msaidizi kwa kikosi cha Jangwani kwa vipindi tofauti jambo ambalo linamfanya aiwe mgeni katika mitaa ya Twiga na Jangwani.

Kocha wa makipa wa timu ya Taifa Tanzania "Taifa Stars" Juma Pondamali "Mensah" anachukua nafasi ya aliyekua kocha wa makipa mkenya Razaki Siwa ambaye pia alistishiwa mkataba wake mwishoni mwa mwaka 2013.


Pondamali golikipa aliyeichezea Yanga miaka ya 80's kwa kwa kiwango cha hali ya juu hata kufikia kuwa katika kikosi cha Tanzania kilichoshiriki mashindano ya Mataifa Afrika nchini Nigeria mwaka 1980, sio mgeni katika timu ya Young Africans kwani awali alishwahi kuwa kocha msaidizi kwa vipindi tofauti.

Dr Suphian Juma anachukua nafasi ya Dr Nassoro Matuzya ambaye pia alisitishiwa ajira yake mwishoni mwa mwaka 2013 pamoja benchi la Ufundi.

Mara baada ya kuwapata viongozi hao watatu wa Benchi la Ufundi kikosi cha Young Africans kesho kitaanza mazoezi jioni katika Uwanja wa Bora Kijitonyama kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya Kimataifa huku kocha Mkwasa akiongoza benchi hilo la Ufundi mpaka atakapopatikana kocha mkuu ambaye watafanya watafanya kazi kwa pamoja

No comments:

Post a Comment