Wednesday, February 19, 2014

Msanii Tiko Hassan atawaka wasanii 'mapepe' kubadilika


MUIGIZAJI filamu maarufu nchini, Tiko Hassan amewataka wasanii wenzake wa kike wabadilike na waepuke matendo machafu ili kulinda hadhi na heshima yao pamoja na kujiweka katika nafasi nzuri ya kulamba tenda za matangazo.
Msanii Tiko Hassan
Tiko aliyeanza kutamba tangu akiwa kundi la Shirikisho Msanii Afrika, alisema baadhi ya wasanii wanajisahau na kujikita kwenye mambo ya upuuzi na kupoteza mvuto na heshima mbele ya jamii na hata taasisi zilizopo nchini.
Alisema taasisi hizo zikiwemo mashirika na makampuni ya umma na yale ya watu binafsi yamekuwa yakishindwa kuwatumia kutangaza bidhaa zao kama ilivyo kwa baadhi ya wenzao wa kiume kwa sababu 'hawajatulia'.
"Hakuna kampuni au taasisi itakayotaka kumtumia msanii asiyejiheshimu kutangaza bidhaa zao kwa sababu itavunja murua na hadhi ya bidhaa na kampuni husika, lazima wasanii wa kike tubadilike na tutulie," alisema.
Alisema, tenda za matangazo zinasaidia kuvuna pato la ziada ambalo lingewafanya wasanii waishi kulingana na hadhi zao kama ilivyo kwa wasanii wa mataifa mengine wanaokimbiza kwa utajiri kwa tenda nje ya sanaa zao.
"Wito wangu wasanii wa kike wajitambue ni nani ndani ya jamii, wajiheshimu na kuwa mfano mbele ya jamii ili kusaidia kushawishi taasisi kuwatumia kwa matangazo na kuwaingizia pato la ziada," alisisitiza.
Staa huyo wa filamu za 'The Living Ghost', 'Devil's Soul', 'Limbwata',' Check in the Bible', 'Melvin' na nyingine alisema kama msanii wa kike havutiwi na vitendo vya wenzake, lakini hana cha kufanya kwa vile vyombo vya kuweza kuwashughulikia wasanii wa aina hiyo vyenyewe vimekaa kimya.
"Wanatuaibisha na kututia aibu, lakini utafanyaje kama vyombo vyenye jukumu la kuwashughulikia vimenyamaza, ila wanakera sana," alisema Tiko.

No comments:

Post a Comment