Sunday, February 2, 2014

Ruvu Shooting yawasemehe akina Maguli, kocha Olaba anena yake


Elias Maguli
WAKATI wachezaji Elias Maguli na Ali Kani wakianza mazoezi na wenzao baada ya kusamehewa na uongozi wa Ruvu Shooting kwa kitendo cha utoro wa kwenda Oman bila ruksa, kocha Tom Olaba amesema anaendelea kuwaangalia kwanza.
Wachezaji hao walitoroka mapema mwezi uliopita kwenda kusaka timu ya kujiunga nayo kwa soka la kulipwa, wakati klabu yao ikijianda na duru la pili na waliporejea uongozi uliwapiga 'stop' kwa kitendo hicho cha utovu wa nidhamu.
Hata hivyo kwa mujibu wa Afisa Habari wa klabu hiyo, Masau Bwire wachezaji hao waliuangukia uongozi kwa kuomba radhi na kuwaomba msamaha wachezaji, makocha na TFF na wao wamewasamehe.
"Tumewasamehe na wamerejeshwa kundini wakianza mazoezi na wenzao tangu Alhamisi na kocha Tom Oloba atakuwa na maamuzi ya kutaka kuwatumia kama watamfaa kwa mechi zijazo," alisema Bwire.
MICHARAZO liliwasiliana na Oloba kwa njia ya simu jana na kukiri kurejea kikosi kwa wachezaji, lakini alisema ni mapema mno kuwaelezea wachezaji hao na kujua kama ataweza kuwatumia katika mechi mbili zijazo za ugenini wiki hii.
Mkenya huyo alisema licha ya wachezaji hao kuanza mazoezi na wenzao tangu Alhamisi, bado anaendelea kuwaangalia  ili kupima uwezo wake na kama wana fiti katika mfumo wake na kuweza kuwatumia kwa mechi hizo zijazo.
"Ni kweli akina Maguli na Kani wameshaanza mazoezi na ninawangalia pamoja na wenzao kuona wachezaji gani nitakaoteua kuondoka nao kwenda Tanga na Mbeya, hivyo naendelea kuwangalia kwanza," alisema Olaba.
Olaba anatarajiwa kuteua kikosi chake kesho saa chache kabla ya safari yao ya Tanga kwenda kuvaana na Mgambo JKT siku ya Jumatano katika uwanja wa Mkwakwani.
Baada ya mechi hiyo timu hiyo itaunganisha hadi jijini Mbeya kucheza mechi yao ya kiporo dhidi ya wenyeji wao maafande wa Prisons kwenye uwanja wa Sokoine.
Mechi yao ya awali iliyokuwa ichezwe Janauri 25 iliahirishwa kutokana na tatizo la uwanja wa Sokoine uliokuwa umefungiwa na TFF kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati.

No comments:

Post a Comment