Sunday, March 30, 2014

Ashanti Utd yawafumua maafande wa Oljoro JKT


Ashanti United ambao wameibuka na ushindi leo dhidi ya Oljoro JKT ya Arusha
 WATOTO wa Jiji, Ashanti United jioni ya leo imezinduka na kufufua matumaini yao ya kubaki katika Ligi kuu Tanzania Bara baada ya kuwacheza kwata maafande wa Oljoro JKT ya Arusha kwa kuwalaza mabao 2-1 katika pambano pekee la ligi hiyo lililochezwa leo.
Pambano hilo lilichezwa kwenye uwanja wa Chamazi na washindi walienda mapumziko wakiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Hassani Kabunda, huku Oljoro wakipoteza penati katika dakika ya tano tu ya mchezo huo.
Kipindi ca pili wenyeji walipata bao la pili lililofungwa kwa mkwaju wa penati na Hassani Kabunda kabla ya Oljoro kujipatia bao la kufutria machozi lililotokana pia kwa mkwaju wa penati kupitia kwa Shaibu Nayopa.
Ushindi huo uliokuwa ukihitajiwa mno na Ashanti umeiwezesha timu hiyo inayonolewa na kocha mahiri, King Abdallah Kibadeni, kufikisha jumla ya pointi 21 kutokana na mechi 23 na kushika nafasi ya 11.
Oljoro ambayo inapigana kuepuka kushuka daraja kama ilivyo kwa wapinzani wao, imeendelea kusota kwenye nafasi ya 13 ikiwa na pointi 16, tatu zaidi ya wanaoburuza mkia Rhino Rangers ambayo kesho itakuwa wageni wa JKT Ruvu kwenye uwana wa Chamazi.
Mechi nyingine zitakazopigwa kesho ni kati ya vinara wa ligi hiyo, Azam itakayokwaruzana na Simba kwenye uwanja wa Taifa, Yanga watakuwa ugenini kuumana na Mgambo JKT, huku mabingwa wa zamani Mtibwa Sugar na Coastal Union watapepetana uwanja wa Manungu, Morogoro na Kagera Sugar itaialika Ruvu Shooting na jiji la Mbeya litashuhudia Mbeya City na Prisons-Mbeya zitaumana uwanja wa Sokoine.

No comments:

Post a Comment