Thursday, March 27, 2014

KAMATI YA UONGOZI WA BARAZA LA VYAMA VYA SIASA YAONYA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA


Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini Peter Kuga Mziray(katikati) akitoa tamko la Kamati ya Uongozi wa Baraza hilo leo mjini Dodoma juu ya mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba ambapo aliwataka kuzingatia kanuni za Bunge hilo zinazokataza vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu ndani ya Bunge. Wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili wa Baraza hilo Nancy Mrikaria(kushoto) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Siasa wa Baraza hilo Rashid Mtuta(kulia)

 (Picha na Maelezo-Dodoma) 

(Na Magreth Kinabo ,MAELEZO Dodoma)
KAMATI  ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa inawaomba wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kuzingatia kanuni  kwani zinakataza vitendo vya utovu wa nidhamu wakati wa vikao vya Bunge hilo .
 Kauli hiyo imetolewa leo mjini  na  Mwenyekiti wa Baraza hilo, Peter Mziray  katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma kufutia baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuonesha vitendo visivyo na nidhamu  ikiwemo kuzomea.    
           
“ Kamati ya  Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa inawaasa wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kubadilika na kuonesha nidamu ambayo Watanzania wote wanategemea kutoka kwao,” alisema Mziray.
 Alisema  Kamati hiyo inaamini kuwa mjumbe anaweza kutoa hoja yake nzito ya kukubali na kupinga jambo ikakubalika au kukataliwa na wajumbe wengine  wengine au Mwenyekiti bila ya kuzomewa.
Aidha Mwenyekiti  huyo Mziray amemtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalum kutoyatambua makundi ya Tanzania Kwanza na UKAWA kwa kuwa sio makundi rasimu ndani ya Bunge hilo na ndio yanasababisha vurugu kwa kuweka maslahi ya vya siasa mbele badala ya Taifa.
Amewataka wajumbe  wa Bunge Maalum la Katiba kuacha kujihusisha na makundi  hayo  badala yake wachambue na kuunga mkono hoja kwa uzito wa hoja na kuzingatia masilahi ya taifa badala ya kuzingatia mtazamo wa kundi fulani. 
Mziray ameongeza kuwa wajumbe wanatakiwa kuepuka vitendo ambavyo vinakwamisha mchakato wa kupata Katiba mpya kwa mustakabali wa taifa hili na Wananchi kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amesema kuwa Kamati ya Uongozi  imeona ni vema wajumbe wa baraza hilo, wakuu wa vyama vya siasa, ambao si wajumbe wa baraza hilo wakutane ili kujadiliana, kushauriana na kuridhiana ili kuweza kufanikisha  azma ya kupatikana kwa Katiba Mpya  kwa mwafaka.

No comments:

Post a Comment