Tuesday, March 18, 2014

Maafa! Nane wafa mgodini wakichimba dhahabu


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiSdFcYwty9B9XpjnDnX7BESYw03rh6lpQPL0-IwljQIDpjBbtc15bUOD0bJrZeBt5aWidisYdh_jUqhrj1LHixWUsdHHe8FkQSdGdZlEHUe74jAxsoxh8fh7yfsP2AOa-0C4tzOC1vYdSJ/s1600/Geita+gold+mine+1.jpg
Picha haihusiani na habari, ila wanaoonekana ni Vijana wakiwa machimboni
WATU wanane wamefariki dunia na moja kunusurika katika machimbo  madogo ya dhahabu yaliyopo vijiji cha Kalole na Nyangalaya kata ya Lunguya  wilayani Kahama, Shinyanga baada ya kuangukiwa na vifusi.
Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Kalole, Furaha Mashamba, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5:00 usiku wakati wachimbaji hao wakiendelea kuchimba dhahabu.
Alisema katika matukio hayo, watu saba walikufa katika machimbo ya kijiji cha Kalole na mmoja   machimbo ya Nyangalata.
Mashamba alisema kuwa baada ya tukio hilo, wakazi wa kijiji hicho walipewa taarifa na kwenda eneo la tukio kujaribu kuwaokoa, lakini ilishindikana.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mtendaji huyo, mmoja wa wachimbaji aliokolewa akiwa hai.
Aliwataja waliofariki ambao ni wakazi wa kijiji cha Kalole kuwa ni Mwadogo Kibasi Kiaka (26), Juma Malingaya (30), Charles Iheyolo (21), Roma Masolwa (26), Juma John (33), Paul James (24), Ngaleba Kacheyekele (24) na Daudi John wa kijiji cha Nyangalata Alimtaja aliyenusurika kuwa ni Michael Pius (43) mkazi wa Morogoro.
Ofisa Mtendaji huyo alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mashimo hayo kutokuwa na usalama wa kutosha na maji kuingia kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha wilayani Kahama.
Kwa upande wake, Ofisa Madini wilayani Kahama, Amir Chande, alisema kuwa machimbo ya kijiji cha Kalole yalishafungwa muda mrefu, lakini wachimbaji wamekuwa wakiyavamia kuendelea na uchimbaji kinyemela.
Chande alitoa agizo kwa wachimbaji ambao bado wapo eneo hilo kusitisha kazi hiyo haraka hadi hapo serikali itakapotoa maelekezo mengine.
“Mnaoendelea kuchimba mpo hapa kimakosa na kwa sababu hakuna mwenye leseni hapa ya uchimbaji wa madini, ni makosa kufanya kazi hii ya uchimbaji na kuanzia sasa machimbo  tunayafunga kwa usalama wenu,” alisema Chande.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa miili ya wachimbaji hao imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa mazishi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment