Monday, March 24, 2014

Mama Pinda: Tamasha laPasaka ni Neema ya Mungu


KUNA njia nyingi ya kumtukuza, kumuabudu na kupata Neema ya Mungu ambayo ni kwenda kanisani na kusali na njia ya nyimbo ambayo mtu unaweza kupata Baraka kubwa kutokana na nyimbo za injili zinazoimbwa na waimbaji mbalimbali wa muziki huo; amesema Mama Tunu Pinda.

Mama Pinda ambaye ni mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Peter Pinda, ameyasema hayo alipozungumza na Hekaheka kuhusu Tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika Aprili 20 mwaka huu ambayo itakuwa  ni Sikukuu ya Pasaka inayoadhimishwa na Wakristo Duniani kote kwa Kufufuka Yesu Kristo mwana wa Mungu.

Akielezea faida za kwenda kwenye Tamasha la Pasaka, Mama Pinda anasema ni kwa ajili ya kwenda kusikiliza nyimbo mbalimbali zitakazokuwa zikiimbwa na waimbaji wa nyimbo za injili ambako unaweza kupata Baraka na kuachana na matendo yasiyompendeza Mungu na hatimaye kutenda dhambi.Tamasha hilo ambalo huandaliwa na kampuni ya Msama Promotions, linatarajiwa kufanyika Jijini Dar es salaam kwa siku hiyo ya Pasaka na hatimaye katika Mikoa mingine saba ya Tanzania Bara.

 “...Mwaka juzi nilipokuja kwenye Tamasha la Pasaka kulikuwa kuna watu wengi wa kila rika wazee, vijana na hata watoto wadogo hali hiyo ilidhihirisha ni kwa namna gani Watanzania wanapenda nyimbo za injili ambazo ninaamini wanapata Neema ya Mungu, alisema Mama Pinda.Akaongeza, “Utamaduni huu wa kusherehekea Sikukuu za kidini kama vile Pasaka kwa kwenda katika matamasha ya nyimbo za injili ni mzuri kwa sababu unawaondoa watu katika vishawishi na kuwafanya kuwa karibu zaidi na uwepo wa Mungu,…”

Amesema ili kupata Neema ya Mungu ni vyema watu wengi zaidi wakajitokeza siku hiyo ya Tamasha la Pasaka kwa Dar es salaam na mikoa mingine ambayo Tamasha litafika ili kuweza kujizolea baraka za Mungu kupitia nyimbo za injili ambazo zitaimbwa na waimbaji wa ndani na nje ya nchi; huku akisisitiza kuwa endapo atapata nafasi kwa mwaka huu atahudhuria tamasha hilo. Hata hivyo alisema nyimbo za injili ni burudani lakini kwa upande mwingine ni sehemu ya ibada ambayo msikilizaji anapokea Baraka na mafundisho ya biblia kupitia nyimbo hizo; lakini pia zinasaidia kutokutenda dhambi kwa kwenda katika starehe ambazo hazimpendezi Mungu.

“…Sikuku ya Pasaka inaadhimishwa kwa Kufufuka kwa Yesu Kristu ambayo ni alama ya ushindi kwa wanadamu, hivyo ni busara kwa Wakristo wote kuhakikisha tunaacha dhambi na kuyashika yale yote aliyotuachia Yesu Kristo, ambayo ni Upendo na Amani bila kusahau kuiombea nchi yetu. 

Tamasha la Pasaka ambalo linatarajiwa kuwashirikisha waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili kutoka ndani na nje ya nchi, lengo kuu ni kuweza kupata fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika vituo vya kulelea yatima, akinamama wajane na wengine wenye uhitaji maalum.

Hata hivyo Mama Pinda aliwataka Watanzania kuwa na Moyo wa kujitoa kwa watu wahitaji ambao wanahitaji misaada mbalimbali na hawana mtu wa kuwasaidia. “…Unaweza kukuta familia moja mtoto anakula chakula mpaka anazasa na kutupwa, lakini familia nyingine mtoto hana chakula na analala njaa; hivyo ni jukumu letu sote kusaidiana kama binadamu, tusiiachie serikali kila kitu ifanye,” alisema Mama Pinda.

Akaongeza kuwa Mkurugenzi wa Msama Promotion Alex Msama, ni mfano mzuri wa kuigwa na  watu wenye uwezo kuwasaidia wahitaji, kwa kufanya hivyo watapata Baraka na kuongezewa zaidi.

No comments:

Post a Comment