Thursday, March 20, 2014

RAIS KIKWETE KULIHUTUBIA BUNGE LA KATIBA MACHI 21


                 
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Iddi  akijadiliana jambo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda(kushoto) wakati wa semina ya kuhusu kanuni za bunge hilo leo mjini Dodoma.
Na Magreth Kinabo,Dodoma

Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuhutubia Bunge Maalum Machi 21, mwaka huu mjini Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu wa bunge hilo,  Yahya Khamis Hamad wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa waandishi wa habari wa ofisi za Bunge mjini Dodoma.

“Kwa mujibu wa kanuni ya 75 (1), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atalihutubia Bunge Maalum siku ya Ijumaa Machi 21 ,mwaka 2014 saa 10:jioni, ambapo wageni waalikwa wote watatakiwa kuwa wameingia na kuketi katika  maeneo watakayoelekezwa saa 9:00 alasiri,” alisema Katibu huyo.

Aidha Katibu huyo alisema ratiba ya shughuli hiyo itaanza na kikao cha Bunge saa 9:10 na baadae kikao hicho kitaanza saa 9:20 kwa ajili ya kumpokea Rais .

 Aliongeza kuwa mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Bunge, Rais Kikwete atapokewa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Naibu Katibu wa Bunge Maalum, ambapo baadae ataelekea katika jukwaa maalum kwa ajili ya kupokea salamu za heshima na kukagua Gwaride Maalum ambalo limeandaliwa na jeshi la polisi.

Baada ya shughuli zote kufanyika katika viwanja vya Bunge kumalizika, utaratibu umewekwa  kwa viongozi kuingia Bungeni kwa maandamano maalum.

Viongozi watakaohusika katika maandamano hayo ni Makamu wa  kwanza wa Rais wa Zanzibar ,Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na hatimaye   Rais Kikwete ambaye atafuatana na Mwenyekiti wa bunge hilo.

Katibu huyo aliwataja viongozi wegine walioalikwa kuwa ni viongozi wa kitaifa na watendaji wakuu kutoka pande zote Muungano, viongozi wa kitaifa wastaafu,ambao ni marais wastaafu kutoka pande zote za muungano, mawaziri wakuu wastaafu, waziri kiongozimstaafu na maspika wastaafu.

Viongozi wengine ni mama Maria Nyerere, Mama Shadia Karume na Mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya  Mabadiliko ya Katiba.

Wageni wengine walioalikwa katika utaratibu huo ni taasisi za dini, zisizozakiserikali, tansia  ya habari, vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu, vyama vya watu wenye ulemavu, wafanyakazi,wafugaji,wavuvi, wakulima na wawakilishi kutoka sekta binafsi.

Kwa  mujibu wa ratiba ya shughuli hiyo Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia bunge hilo kwa muda wa saa moja. Hivyo shughuli hizo zitakamilika majira ya saa 12:00jioni.

No comments:

Post a Comment