Thursday, April 17, 2014

HATIMAYE WASHINDI WATATU WA SHINDANO LA TANZANIA MOVIE TALENTS KANDA YA KATI WAPATIKANA



Na Josephat Lukaza wa Proin Promotions Limited - Dodoma

Hii ni baada ya washindi watatu kutoka Kanda ya Kati kupatikana katika shindano la kusaka vipaji vya kuigiza lililoendeshwa na Kampuni ya Proin Promotion Limited (PPL). Fainali ya kuvisaka vipaji kwa kanda ya Kati  ilifanyika jana Mnamo tarehe 15 April 2014 Mkoani Dodoma na washindi kutangazwa na Jaji Mkuu wa shindano hilo, Roy Sarungi aliyesaidiwa na Yvonne Chery ‘Monalisa’ na Single Mtambalike ‘Richie Richie.’

Roy kwa kusaidiana na Yvonne Chery ‘Monalisa’ na Single Mtambalike ‘Richie Richie.’ aliwatangaza Joyce Rebeca, Moses Obunde na Mwinshehe Mohamed kuwa washindi wa shindano la kusaka vipaji vya kuigiza Tanzania lijulikanalo kama Tanzania Movie Talents ambapo kila mmoja alipewa zawadi nono ya Sh 500,000. Shindano hilo liliwashirikisha washiriki 500, lakini ni washiriki watano wenye vipaji waliofanikiwa kuingia tano bora na baadaye majaji walifanya kazi kubwa ya kuwachagua na kuwatangaza washindi watatu.

Mshiriki mkubwa kuliko wote , Idrisa Ally  (40), alionesha kipaji cha hali ya juu cha kuigiza na alizawadiwa na majaji Sh 100,000. Idrisa hatakwenda kushiriki fainali za mashindano hayo zinazotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu jijini Dar es Salaam kutokana na umri wake kuwa mkubwa kuliko kigezo cha umri kilichowekwa cha kuanzia miaka 14 hadi 35, ingawa majaji waliahidi kuwasiliana naye kwa lengo la kuendeleza kipaji chake umri wake utakaporuhusu.

“Tumebaini kuwa Kanda ya Kati hususani Mkoa wa Dodoma kuna vipaji vingi vya sanaa ya uigizaji na katika hili Idrisa Ally ametuthibitishia yeye ni mzee mwenye kipaji, lakini amedhihirisha kuwa ana kipaji cha kuigiza,” anasema Jaji Mkuu wa shindano hilo, Sarungi anasema sanaa ya uigizaji ni muhimu kwa vijana, kwa vile sasa hutoa fursa ya ajira ambapo imewawezesha vijana wengi nchini kujiajiri wenyewe na kuimarika kiuchumi.

“Ni matumaini yangu kuwa kwa washindi hawa wa Kanda ya kati hawataishia hapa watajiendeleza zaidi kwani uigizaji sasa ni ajira,” anasema. Mshiriki Moses Obunde  alishindwa kuzuia furaha yake baada ya kutangazwa mshindi, aliangua kilio kuashiria furaha aliyokuwa nayo na kuufanya ukumbi mzima kutaharuki.
Ofisa Uhusiano wa Proin Promotion Limited (PPL), Josephat Lukaza, ambao ndio waratibu na waandaaji wa shindano hilo la kusaka vipaji vya uigizaji, anasema mashindano hayo yanaendeshwa kikanda, ambapo kwa kuanzia walianza kusaka vipaji kwa Kanda ya Ziwa na Kumalizika Jana katika Kanda ya kati Mkoa wa Dodoma na hatimaye zoezi hili kuamia Kanda ya Juu Kusini ambapo usaili utafanyika Mkoani Mbeya kuanzia tarehe 19 April.

“Baadaye tutaelekea Kanda ya Njanda za Juu Kusini lakini tunashukuru kwa ushirikiano tulioupata kwa wakazi wa Kanda ya Kati, tumepata washiriki 600, ambao tuliwachuja hadi kuwapata washindi watatu waliokidhi vigezo tulivyovihitaji,” anasema Lukaza. Baadhi ya vigezo kwa mujibu wa Lukaza, vilikuwa ni mshiriki kuwa na umri kuanzia miaka 14 hadi 35, anayejiamini, mbunifu, anayemiliki jukwaa na igizo lake libebe ujumbe wa kuelimisha.

Anasema lengo la PPL kuzungukia kanda hizo sita nchini ni kuhakikisha kuwa inavisaka vipaji vya vijana kupitia sanaa ya maigizo, ambavyo vimejificha ili viendelezwe na kampuni yake. “Tumeamua kuwekeza katika sanaa maana sanaa ni fursa kama zilivyo fursa zingine nchini na ni matumaini yetu kuwa jamii itatuunga mkono katika safari ndefu tuliyo nayo ya kuvisaka na kuviendeleza vipaji,” anaeleza ofisa huyo uhusiano.
Anasema PPL inaendesha shindano hilo kwa kanda sita nchini ambazo ni Kanda ya Ziwa, Magharibi, Pwani, Kati, Kaskazini na Kusini.

“Kwa sasa tumeanza na mikoa sita, lakini matarajio yetu ya baadaye ni kuifikia mikoa yote nchini ambapo tunaamini kuna vipaji vingi vya wasanii vimejificha ili waweze kupata ajira kupitia vipaji vyao,” anasema na kuongeza kuwa mshindi wa jumla baada ya mashindano ya kikanda kumalizika atapatikana Agosti mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambako ataondoka na zawadi nono ya Sh milioni 50.

Anasema usakaji vipaji hivyo huendeshwa kwa umakini na umahiri mkubwa kupitia kwa majaji na watu wenye utalaamu wa tasnia ya filamu na teknolojia ya habari (IT) walio chini ya kampuni yake, ambao pia huzingatia miiko na maadili ya kazi hiyo kwa kila mshiriki. Anasema PPL imesajiliwa rasmi mwaka 2013 kupitia Sheria ya Usajili wa Makampuni ambayo hushughulika na ukuzaji wa sanaa ya filamu nchini.

“Pia tunashughulika na usimamizi wa uzalishaji wa filamu nchini, uzalishaji na usambazaji wa DVD na filamu zilizokamilika kuingia sokoni na matarajio yetu ya baadaye ni kuwa kampuni bora katika Bara la Afrika,” anaeleza. Wakizungumza na gazeti hili, washindi waliobuka kidedea waliwashukuru waandaaji wa shindano hilo kwa kuibua vipaji vyao ambavyo wanasema visingeweza kutambulika.

Crecensiah anasema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwibua katika shindano hilo na kumwezesha kuwa mshindi, ambapo sasa anaamini kuwa ndoto yake ya kuwa msanii wa kimataifa imetimia. “Namshukuru Mungu kwa yote, lakini zaidi niwashukuru waandaaji wa shindano hili kwa kutumia muda wao na fedha kuvisaka vipaji, binafsi naona kiu yangu ya kuwa muigizaji wa kimataifa imetimia, nitaongeza juhudi kubwa katika tasnia ya filamu,” anasema msanii huyo. Naye Janeth anasema penye nia pana njia, kwa madai kuwa alikuwa na kiu ya kuwa msanii wa kuigiza kwa muda mrefu hasa baada ya kuwaona wasanii mbalimbali kupitia luninga nchini.

“Kwa kweli naweza kusema nimepata maji ya kunywa dhidi ya kiu yangu ya kuwa msanii, ni kazi ambayo nilikuwa naipenda tangu nikiwa mtoto namshukuru sana Mungu na waandaaji wa shindano hili la kusaka vipaji vya kuigiza,” anaeleza mshindi huyo. Kwa upande wake, Joshua Wambura anasema ushindi wake ni mwanzo wa safari yake ndefu katika kuingia katika tasnia ya filamu ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment