Wednesday, April 9, 2014

Vitu Vizito kuendesha harambee kusaka fedha za kwenda Botswana


Baadhi ya viongozi wa TAWA akiwemo Katibu Mkuu Magnus Simon (aliyeshika dambeli) wakiwa na baadhi ya wachezaji katika ukumbi wa Mayfair Plaza
Baadhi ya viongozi wa TAWA wakiwa na wachezaji wa mchezo huo wa kunyanyua vitu vizito
Rais wa Shirikisho la Wanyanyua Vitru Vizito Mr Kyler toka Marekani ( wa pili toka kulia) akiwa na baadhi ya wachezaji wa Tanzania alipotembelea hapa nchini hivi karibuni.
Wachezaji wa timu ya taifa wa mchezo huo wakionyesha umwamba mbele ya viongozi wa TAWA
Tupo fiti kinoma...tupelekeni Botswana tukalete medali
Titus Joseph akijiandaa kunyanyua chuma mbele ya wenzake
Katibu Msaidizi wa TAWA, Hillary Kahinji (wa kwanza kushoto mbele) akifanya mazoezi na wachezaji wa timu ya mchezo huo kwenye ukumbi wa Mayfair Plaza
Mkurugenzi wa Idara ya Michezo nchini, Leonard Thadeo ( wa pili toka kushoto) akiwa na viongozi wa TAWA mara baada ya kuchaguana mwezi uliopita.
 CHAMA cha Wanyanyua Vitu Vizito Tanzania (TAWA) kimeandaa hafla maalum itakayotumika kuendesha harambee ya kusaka fedha za kuiwezesha Timu ya Taifa ya mchezo huo kwa Vijana kwenda kwenye michuano ya Afrika itakayofanyika nchini Botswana mwezi ujao.
Katibu Mkuu wa TAWA, Magnus Simon, aliiambia MICHARAZO kuwa, hafla itakayoambatana na uzinduzi wa chama hicho kilichofufuliwa upya itafanyika siku ya Mei 3 mwaka huu kwenye ukumbi wa Mikocheni Resort, ambapo wanatarajiwa wageni mbalimbali na wadau wa mchezo huo watahudhuria.
Simon alisema wamekusudia kukusanya si chini ya Sh. Milioni 20 zinazoweza kuwasaidia kupeleka kikosi cha wachezaji watano katika michuano hiyo ya Vijana ya Afrika itakayofanyika Botswana kati ya Mei 22-26.
"Baada ya kukwama kutuma timu katika michuano ya Afrika kuwania kucheza michezo ya Olmpiki kwa vijana nchini Cameroon, tunapigana angalau tuweze kutuma timu Botswana na tumeandaa hafla itakayoambatana na harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya jambo hilo," alisema Simon.
Simon, alisema hafla hiyo mbali na kuendeshwa kwa harambee pia itapambwa na mazoezi na shindano ndogo la wanyanyua vitu vizito na wale ambao watafanya vyema watazawadiwa pamoja na kuongezwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, kinachoendelea kujifua kwenye ukumbi wa Mayfair Plaza.
Katibu alisema wachezaji hao wa taifa ndiyo pia watakaokuwa sehemu ya watakaoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa baadaye nchini China na Uganda.
Simon alisema mpaka sasa TAWA imefanikiwa kupata wadhamini wachache ambao ni Akbar Jaffer wa Mayfair Plaza,  Mikocheni Resort Centre (MRC), Saada Beauty Para na blogu hii (MICHARAZO MITUPU)ambao wamekuwa bega kwa bega na uongozi waop katika kukirejesha chama chao katika uhai baada ya kuwa kimya kwa miaka 9 na kuwaomba wengine wajitokeze kwa ajili ya kufanikisha hafla hiyo ya Mei 3.
"Tunayaomba makampuni, asasi na watu binafsi watusaidie tufanikishe hili, ili Tanzania tukashiriki michuano hiyo na kurejesha heshima katika anga la kimataifa baada ye soka na michezo mingine kukwama kusuuza nyoyo za mashabiki," alisema Simon.

No comments:

Post a Comment