Saturday, April 26, 2014

WANAVIJIJI MBEYA WALAUMIANA UDHIBITI MIMBA KWA WANAFUNZI‏


Baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha Usoha Njiapanda, Wilaya ya Mbeya Vijijini wakizungumza katika mkutano na mwandishi wa habari hizi juu ya changamoto anuai za huduma za kijamii kijijini hapo.
Baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha Usoha Njiapanda, Wilaya ya Mbeya Vijijini wakizungumza katika mkutano na mwandishi wa habari hizi juu ya changamoto anuai za huduma za kijamii kijijini hapo.Mwenyekiti wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Willson Mwamunyila (katikati) pamoja na wanakijiji wenzake wakizungumza na mwandishi wa habari hizi. Mwenyekiti wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Willson Mwamunyila (katikati) pamoja na wanakijiji wenzake wakizungumza na mwandishi wa habari hizi. Mratibu wa Elimu Kata ya Tembela, Antony Mwaikwila akizungumza na mwandishi wa habari hizi. Mratibu wa Elimu Kata ya Tembela, Antony Mwaikwila akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
WANAVIJIJI wa vijiji vya Shibolya, Usoha Njiapanda, Simambwe, Ikhoho na Ilembo Usafwa vyote vya wilayani Mbeya Vijijini wametupiana lawama kuhusiana na baadhi ya wazazi na viongozi wa vijiji kuwa wakifumbia macho watu wanaotuhumiwa kuwatia mimba wanafunzi wa msingi na sekondari na kuwakatisha masomo.
Kauli hiyo imetolewa juzi na baadhi ya wanakijiji walipokuwa wakifanya mazungumzo na mwandishi wa habari hizi Wilaya ya Mbeya Vijijini kwa vyakati tofauti alipotembelea vijiji hivyo kuangalia changamoto za elimu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanavijiji walisema idadi kubwa ya wanafunzi wanaotiwa mimba na kukatishwa masomo ya shule za msingi na sekondari wamekuwa wakirudi vijijini na kulea watoto huku kukiwa hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa kwa wanaotuhumiwa kuwatia mimba.
Greyson Ngolia wa Kijiji cha Shibolya alisema katika kijiji hicho wapo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao wanalea watoto wao baada ya kutiwa mimba na kukatiswa masomo yao.
“…Hapa kijijini tunao hadi wanafunzi wa shule za msingi ambao wametiwa mimba na kukatishwa masomo, wanalea watoto wao nyumbani hakuna hatua zozote zinazochukuliwa iwe kwa mzazi wala waliowatia mimba na wengine wapo hapa hapa,” alisema Ngolia.
Eliud Mwakilasa mkazi wa Kijiji cha Usoha Njiapanda alisema katika kijiji hicho hakuna hatua zinazochukuliwa kwa wanafunzi wanaopata mimba kuanzia kwa viongozi wa kijiji, wazazi na wala uongozi wa shule husika anaposoma mtoto.

Naye Maria Kolneri wa Kijiji cha Usoha Njiapanda alisema katika kijiji hicho hakuna utamaduni wa kuwashtaki watu wanaotuhumiwa kuwatia mimba wanafunzi na suala hilo linaogopwa na kila mmoja kwa kile kuhofia kutengwa.
“…Hapa kijijini hakuna utaratibu huo wa kuwashtaki waliowatia mimba wanafunzi watu wanaogopa kulaumiwa kuanzia viongozi wa kijiji na hata wazazi wa mtoto anayekuwa ametiwa mimba, kiujumla tunaogopana,” alisema Bi. Kolneri.
Faustina Nafasi toka Kijiji cha Simambwe alisema idadi kubwa ya wanafunzi wanaopata mimba usababishwa na umbali wa shule wanazosoma, ambapo baadhi yao wamelazimika kupanga kwenye vyumba karibu na shule (yaani mageto) jambo ambalo linachangia idadi kubwa kurubuniwa kwa kukosa uangalizi wa karibu toka kwa wazazi/walezi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Willson Mwamunyila alikiri kuwepo na matukio ya kesi za mimba kwa wanafunzi katika eneo lake na vijiji vinavyomzunguka lakini alisema hali ya kushindwa kuwashughulikia wanaowatia mimba wanafunzi huchangiwa na ushirikiano mdogo toka kwa wazazi wa watoto.
“…Unakuta umeletea taarifa ya mimba kwa mwanafunzi toka shuleni, ukienda kwa mzazi anasema hajui aliyemtia mimba mwanaye na vile vile mtoto anasema aliyempa mimba hamjui sasa mazingira kama hayo mnashindwa pa kuanzia, maana hakuna ushirikiano…wawazi na wanafunzi binafsi ndio nawaona kikwazo,” alisema Mwamunyila.
Kwa upande wake Mratibu wa Elimu Kata ya Tembela, Antony Mwaikwila alikiri uwepo wa matukio ya mimba katika shule anazozisimamia na takwimu zimekuwa zikitofautia kila mwaka, licha ya kesi nyingi kushindwa kushughulikiwa kwa kile kukosa ushirikiano.
Alisema kesi nyingi hata zikifika polisi huishia kituoni maana wanafunzi wengi wanaotiwa mimba hudai hawawajui waliowapa mimba hivyo kukosa ushahidi. “…Mfano mwaka 2013 Shule ya Sekondari Shibolya tulipata taarifa ya mimba tatu lakini watoto walipinga kuwa hawawajui waliowapa mimba hivyo kesi kuishia njiani, zipo kesi zinafunguliwa lakini zinaishia njiani kwa kukosa ushahidi.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TGNP

No comments:

Post a Comment