NA MWANDISHI WETU
TIMU ya soka ya Kurugenzi Mufindi iliyopo Ligi Daraja la
Kwanza, imejipanga vilivyo kuhakikisha inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu
wa mwaka 2015/16.
Meneja wa timu hiyo, Athuman Kihamia ambaye ni Mweka Hazina
wa Halmashauri wa Wilaya ya Mufundi, ameliambia gazeti hili jijini Dar es
Salaam jana kuwa wameunda uongozi mpya ili kufanikisha azma ya hiyo.
Alisema kuwa viongozi hao ni watumishi wa Halmashauri hiyo ya
Wilaya Mufindi, wamiliki wa timu hiyo ambayo msimu uliopita ilipambana vilivyo,
lakini ilishindwa kupanda daraja kutokana na sababu mbalimbali.
“Viongozi wote wametoka Halmashauri ya Wilaya ya Mufundi kwa
sababu ndiyo inayoigharamia timu kwa kila kitu, lakini tutaunganana viongozi
wengine wawili, Mweka Hazina na Katibu Msaidizi watakaopendekezwa na Chama cha
Soka Wilaya ya Mufundi,” alisema Kihamia ambaye ni mmoja wa wadau maarufu wa
soka jijini Dar es Salaam, kwa sasa akiwa ni mtumishi wa halmashauri hiyo.
Kihamia alisema uamuzi huo wa kuunda uongozi mpya, ulifikiwa
katika kikao chao cha Juni 17, mwaka huu ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri hiyo, Paul Ntinika, amepania kuifikisha mbali timu hiyo, ikiwa ni moja
ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi-kuendeleza michezo kwa vijana kama
sehemu ya kukabiliana na tatizo la ajira hapa nchini.
Aliwataja viongozi wapya wa timu hiyo na nafasi zao kwenye
mabano kuwa ni Ofisa Utumishi na Utawala Monica Andrew (Mwenyekiti), Mhandisi
Ujenzi Peter Mawere (Makamu Mwenyekiti), Ofisa Mipango Miji Bernard Kajembe (Katibu
Mkuu) na Mweka Hazina Athuman Kihamia (Meneja).
“Mwenyekiti Monica amechaguliwa kutokana na uzoefu wake
katika soka kwani ni mmoja wa waasisi wa timu ya Mbeya City inayotesa Ligi Kuu
kwa sasa,” alisema Kihamia na kusisitiza kuwa watafanya usajili wa nguvu kufanikisha
azma yao ya kuifanya Mufindi kuwa na timu Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment