Sunday, June 15, 2014

MAMA SALMA KIKWETE AITAKA JAMII KUJENGA TABIA YA KUCHANGIA DAMU KWA HIYARI.


Jamii imetakiwa kujenga tabia ya kuchangia damu kwa hiari kitendo ambacho kitapunguza  vifo vya kina mama wajawazito 363 vinavyotokea kila mwaka kutokana na tatizo la ukosefu wa damu wakati wa kujifungua. 

Mwito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi wa mkoa wa Kigoma kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wachangia damu Duniani zilizofanyika kitaifa mkoani humo.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema takwimu zinaonyesha kuwa takribani wanawake 454 kati ya vizazi hai laki moja hufa kila mwaka kutokana tatizo la uzazi na asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa na ukosefu wa damu.

“Ni dhahiri vifo vinavyotokana na uzazi viko juu na kwa bahati mbaya waathirika wakubwa ni wasichana chini ya umri wa miaka 15, makundi mengine yanayohitaji kuongezewa damu ni kina mama wajawazito wakati wa mimba na kujifungua , watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa ukosefu wa damu unaosababishwa na malaria kali na magonjwa mengine, ajali, wagonjwa wa saratani, upasuaji mkubwa wa moyo, anemia, seli mundu na hemophilia.

Ni wajibu wetu sote kuhakikisha kwamba tunatoa damu ili jamii yetu iweze kutimiza mahitaji yake kwani tunapokuwa na akiba ya damu iliyo salama tunajihakikishia tiba ya ndugu zetu pale wanapopata matatizo bila ya siye kulazimika kutoa damu ya papo kwa hapo”, alisema Mama Kikwete. 

Mwenyekiti hiyo wa WAMA alisema mtu yeyote mwanamke au mwanaume anaweza kuchangia damu ikiwa ana afya njema, umri kati ya miaka 18 hadi 65, uzito usiopungua kilo 50, uwingi wa damu zaidi ya gramu 12 kwa desilita, kutokuwa na shinikizo la damu na kwa mwanamke asiwe mjamzito au ananyonyesha.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii  Dkt. Stephen Kebwe alisema tangu kuanzishwa kwa mpango wa damu salama mwaka 2004 kumekuwa na ongezeko la wachangia damu kwa hiari kutoka kiasi cha chupa 5000 kwa mwaka 2005 hadi chupa 160000 kwa mwaka 2013.

“Changamoto zinazoukabili mpango huu ni mahitaji makubwa kuliko upatikanaji wa damu inakadiriwa  mahitaji ya damu kwa mwaka kitaifa ni wastani wa  chupa 400000 hadi 450000, uelewa mdogo wa jamii kuhusu suala zima la uchangiaji damu kwa hiari, uuzwaji wa damu usio halali Hospitalini jambo ambalo linakatisha tamaa wachangia damu wa hiari na matumizi yasiyo sahihi ya damu katika Hospitali”, alisema Dkt. Kebwe.

Naibu waziri huyo wa Afya na Ustawi wa Jamii alisema mpango wa taifa wa damu salama unaendelea kufanya kampeni ya kuhamasisha uchangiaji wa damu katika jamii, kuendelea kujenga vituo vidogo vya kuchangia damu,  kutoa majibu, nasaha, na malezi kwa wiki mbili mpaka nne baada ya mtu kuchangia damu na kuongeza mazao mbalimbali ya damu. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali Mstaafu Issah Machibya aliwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kujitoa kwao katika zoezi zima la uchangiaji wa damu salama na kuweza kukusanya chupa 3620 kwa kipindi cha wiki tatu  kabla ya kilele cha maadhimisho hayo na hivyo kuvuka malengo kwa asilimia 121 kwani kabla ya kuanza kwa zoezi hilo walijipangia kukusanya chupa salama za damu 3000.

“Mkoa wa Kigoma hupata Damu salama kutoka kituo cha Kanda ya magharibi kilichopo Tabora, umbali wa karibu Km 450 kutoka Kigoma mjini. Ambapo pia upatikanaji wa damu salama umekuwa hautoshelezi mahitaji halisi ya Kimkoa yanayokadiriwa kuwa chupa 22000 kwa mwaka”, alisema Kanali Mstaafu Machibya. 

Alisema ili kukabliana na tatizo hilo  Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na wadau wengine wa maendeleo uliamua kujenga kituo kidogo cha Damu Salama katika eneo la Hospitali ya Maweni  ujenzi wa kituo hicho ambacho kikikamilika  kitaboresha upatikanaji wa damu ndani ya Mkoa na kuboresha utoaji wa huduma za afya umeshaanza na utakamilika ndani ya wiki mbili zijazo. 

Katika maadhimisho hayo Mama Kikwete alizindua mfumo wa kiektronic wa kuhifadhi kumbukumbu za wachangia damu nchini. Pia alitoa kikombe kwa mshindi wa kitaifa kwa mwaka 2013/14 cha sisi ni mashujaa tumeokoa maisha  na cheti kwa Shule ya Sekondari ya Bihawana iliyopo mkoani Dodoma kwa  kutoa chupa nyingi za damu kwa mkupuo  ukilinganisha na idadi ya wananchi waliokuwepo na katika ngazi ya mkoa kikombe kidogo kama hicho kilienda kwa Shule ya Sekondari Kasulu.

Mke huyo wa Rais pia alitoa cheti kwa mwanaume  aliyechangia damu nyingi kuliko wote nchini kwa mwaka 3013/14  hii ikiwa ni mara 53 katika maisha yake Emmanuel Essay kutoka  mkoa wa Kilimanjaro  na kwa upande wa mwanamke cheti hicho kilienda kwa Restituta Mushi kutoka mkoa wa Mwanza ambaye amechangia mara 28.

Mganga  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Leonard Subi alitambuliwa na mpango wa damu salama kwa mwaka 2013/2014 na kupewa cheti kutokana na juhudi za ziada alizozifanya   za kufuatilia upatikanaji wa damu katika Hospitali zake, kwa kushirikiana na mpango wa Taifa wa Damu salama ameweza  na kuhamasisha Halmashauri kutenga bajeti ya kukusanya damu salama na amefanikisha ujenzi wa kituo kidogo cha kukusanyia damu.

Siku ya wachangia damu Duniani ambayo  Kauli mbiu ya mwaka huu ni DAMU SALAMA UHAI WA MAMA ni ukumbusho wa siku ya kuzaliwa kwa Karl Landsteiner  ambaye ndiye aliyegundua mfumo wa makundi yay a damu A, B na O na alizawadiwa tuzo ya Nobel kutokana na ugunduzi huo.
Na Anna Nkinda – Maelezo, Kigoma

No comments:

Post a Comment