Jeshi
la Polisi Tanzania linapenda kutoa shukrani za dhati kwa wananchi wote,
vyama vya siasa, taasisi mbalimbali za serikali, madhehebu ya dini,
asasi za kiraia na vyombo vya habari kwa ushirikiano wa dhati katika
kusimamia masuala ya amani na usalama hapa nchini.
Tunapoelekea
kipindi hiki cha kusherehekea sikukuu ya Eid-El-Fitr, Jeshi la Polisi
linatoa wito kwa wananchi wote kuwa makini na kusheherekea sikukuu hiyo
kwa amani na utulivu pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu
wa amani.
Ikumbukwe
kuwa, wananchi wenye imani ya kiislam na hata madhehebu mengine hutumia
muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye
maeneo mbalimbali ya starehe. Uzoefu umeonyesha kuwa baadhi ya watu
hutumia kipindi hicho cha sikukuu kama mwanya wa kufanya matukio ya
uhalifu kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu.
Jeshi
la Polisi linapenda kuwaondoa hofu wananchi wote kuwa, limejipanga
kikamilifu kuhakikisha wananchi kote nchini wanasherekea sikukuu hiyo
kwa amani na utulivu. Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya
kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote,
aidha, tunapenda kuwatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia
barabara, kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na
hasa kwa madereva wa magari na pikipiki kuepuka kwenda mwendo kasi na
kutumia vilevi wawapo kazini.
Katika
kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo
wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu
kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha
kwa kujaza watu kupita kiasi.
Jeshi
la Polisi linapenda kuwashukuru wale wote ambao tayari wamefunga kamera
za CCTV katika maeneo yao ya starehe, hususani yale yanayokuwa na
mikusanyiko mikubwa ya watu, yakiwemo maduka, hoteli na maeneo ya benki.
Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasisitiza wale ambao bado
hawajaweka kamera hizo, kuweka ili ziweze kusaidia kubaini wahalifu na
hata kurahisisha ukamataji endapo uhalifu unatokea.
Vilevile,
wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto, ili kuepuka ajali
na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao.
Aidha
wananchi wachukue tahadhari watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba
wazi ama bila mtu na watoe taarifa kwa majirani zao, na pale
wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe
taarifa haraka kwenye vituo vya Polisi vilivyo karibu nao au kwa namba
ya simu ifuatayo 0754 785557, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa
haraka.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba - SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment