Thursday, October 23, 2014

SEMINA SIKU YA MSANII KUFANYIKA KESHO


SEMINA ya wasanii mbalimbali iliyoandaliwa na Kamati ya Siku Ya Msanii itafanyika kesho Alhamisi katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa Mjini Dar es Salaam.

Ofisa Uhusiano wa Siku Ya Msanii, Petter Mwendapole alisema maandalizi yote kwa ajili ya semina hiyo yamekamilika na kwamba wasanii 400 mpaka jana walikuwa wameshajiandikisha.
“Lengo letu ni kuwaelimisha wasanii katika kazi zao, lakini pia kuweza kuwapa nafasi ya kupata mafunzo yatakayowasaidia uzeeni wakati ambapo hawatakuwa wakifanya tena sanaa,” anasema.
Mada zitakazowasilishwa ni pamoja na Urasimishaji wa Tasnia ya Sanaa nchini itakayowasilishwa na mtaalamu kutoka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na  Umuhimu wa hifadhi ya jamii kwa wasanii itakayowasilishwa na Mfuko wa Pensheni wa PSPF.
“Mada hizi zimelenga kuongeza uelewa wa wasanii kuhusu umuhimu na ushiriki wao katika sekta ya hifadhi ya jamii na vilevile umuhimu wa kurasimisha sekta ya sanaa nchini. Wasananii kama wadau wakuu wa sanaa, ushiriki wao katika mchakato huu ambao kwa sasa unajumuisha saa ya filamu na muziki pekee ni muhimu sana hivyo semina hii itawapa fursa maridhawa ya kufahamu mengi kuhusu suala zima za urasimishaji katika sanaa”  anasema.
Mwendapole anasema pia suala la haki miliki litakuwa miongoni mwa mada ambazo zitafundishwa kwenye semina hizo kwani suala hilo bado ni tatizo.Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja Mashirikisho ya Sanaa Tanzania, Godfrey Ndimbo alisema  semina ya Siku Ya Msanii itaweza kutoa mwanga kwa jinsi gani wasanii wanaweza kujikwamua katika kwa kutambua nafasi yao katika kutetea haki zao.
Mgeni rasmi katika semina hiyo atakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana,Habari,Utamaduni na Michezo Bi Sihaba S Nkinga. Wadau wengine watakaohurudhuria ni pamoja na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na BASATA.Semina hii ni utangulizi wa kilele cha cha Tuzo za Siku ya Msanii zitakazofanyika siku ya Jumamosi 25/10/2014 katika ukumbi wa Mlimani City

No comments:

Post a Comment