Saturday, November 29, 2014

ASKOFU KILAINI, NZIGIRWA WAZUNGUMZIA TUHUMA

Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini.
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini amekiri kupokea Sh80.5 milioni kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engeering, James Rugemalira akisema si mara yake kwa kwanza kupokea fedha kutoka kwa mfanyabiashara huyo kwa kuwa mara nyingi huwa anachangia kwa uwazi miradi ya jamii.
Askofu huyo alikuwa akizungumzia Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iliyosomwa bungeni juzi ikimtaja kuwa ni miongoni mwa viongozi wa dini na watu wengine waliopokea mabilioni kutoka katika akaunti ya escrow.
Mkurugenzi wa VIP Engeering, James Rugemalira.
Katika ripoti hiyo, Zitto aliwataja viongozi wengine wa dini walioingiziwa fedha katika Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki kuwa ni Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimanye Simon (Sh40.4 milioni).
Akizungumza kwa simu jana, Askofu Kilaini alisema Rugemalira hupendelea kuchangia kwa uwazi miradi ya kijamii na si yeye peke yake aliyempatia mchango, bali kuna watu wengine wengi ambao wameshampatia na kazi yake ni kuipokea na kuifikisha sehemu husika.
Hata hivyo, kabla hajafafanua zaidi hoja yake, simu ilikatika na baadaye hakupatikana tena.
Hata hivyo, jana askofu huyo alinukuliwa na Gazeti la Mawio toleo la jana akisema fedha alizozipokea kutoka kwa Rugemalira ni kwa ajili ya miradi mbalimbali inayoendeshwa na Kanisa Katoliki.
“Ndiyo nimepokea fedha kutoka kwa James na hii siyo mara ya kwanza, kwani mara nyingi amekuwa akichangia miradi mbalimbali ya kijamii,” alisema Askofu Kilaini.
Alipotakiwa na gazeti hilo kuwataja wengine waliochangia kanisa lake na kama nao wamechanga kutoka kwenye fedha za akaunti ya escrow, alisema yeye hayumo kwenye michango hiyo.
Alipoulizwa anawezaje kusema hayumo kwenye orodha ya waliopewa fedha kutoka akaunti ya escrow wakati anakiri kuwa aliingiziwa mamilioni ya shilingi na Rugemalira, alisema michango inayoletwa kwake haina siri, hivyo wezi halisi ndiyo wakamatwe.
“Michango inayoletwa kwangu haina siri, shikeni wezi halisi,” alisema.
Askofu Nzigirwa
Kwa upande wake, Askofu Nzigirwa ambaye alirithi kiti cha Kilaini, cha Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam ameeleza kushtushwa kwake na ripoti ya PAC iliyomtaja yeye na Kilaini kuhusika katika uchotwaji wa Sh306 bilioni za escrow.
Hata hivyo, kiongozi huyo alisema anaandaa taarifa itakayofafanua kwa kina namna ambavyo fedha hizo zinazodaiwa zilitoka katika akaunti ya escrow zilivyoingizwa katika akaunti yake pamoja na hoja na maswali mengi yanayoulizwa na wananchi hasa waumini wa Katoliki kuhusiana na tuhuma hizo.
“Hizo taarifa zimenishtua sana. Bado nashangaa inakuwaje mimi naambiwa nimechota fedha kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow,” alisema Nzigirwa alipokuwa akizungumza na gazeti hili jana.
Nzigirwa alisema anachofahamu hadi sasa fedha zilizoingizwa katika akaunti yake hazihusiki na escrow lakini atafanya uchunguzi ili kupata undani wa fedha hizo na majibu yote yatakuwa katika taarifa atakayoitoa kwa vyombo vya habari siku yoyote kuanzia leo.
(CREDIT: MWANANCHI)

No comments:

Post a Comment