Balozi Alexander A. Muganda, Mwenyekiti mpya Bodi ya
Wakurugenzi ya STAMICO
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
amemteua Balozi Alexander A. Muganda kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) akichukua nafasi iliyoachwa na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Bodi Bw. Rumisha H. Kimambo aliyestaafu kwa hiari.
Rais Kikwete amefanya uteuzi
huo kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 6 namba (2) (b) cha
Tamko la Rais namba 163 la Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1969
iliyotolewa tarehe 18 Agosti 1972. Sheria hiyo inamwezesha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kumteua Mwenyekiti wa Bodi wa Mashirika ya Umma.Uteuzi huo
wa Balozi Muganda unaanzia mwezi Juni, 2014 alipostaafu Bw. Kimambo hadi
Aprili, 2015 muda wa Bodi hiyo utakapoisha.
Uteuzi wa Balozi Muganda
unatokana na utendaji wake mzuri wa kazi na imani kubwa aliyonayo Mheshimiwa Rais.
Kabla ya uteuzi huo, Balozi Muganda
alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO kuanzia Mei, 2013 hadi
alipopata uteuzi huo.
Balozi Muganda ameshika
nyadhifa mbalimbali katika utumishi Serikalini kwa miaka 35 iliyopita, mpaka
hapo alipostaafu rasmi katika utumishi wa umma mwezi Novemba mwaka 2006.
Nyadhifa alizowahi kushika Balozi
Muganda ni pamoja na Mwanasheria wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (1971 –
1976); Mkurugenzi Msaidizi wa Kikosi cha Kupambana na Rushwa (1976-1979); Naibu
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (1980 – 1997); na Balozi wa Tanzania
nchini Zimbabwe na Rwanda (1997-2006).
Balozi Muganda amebobea
katika fani ya Sheria kwa miaka 39 sasa, ambapo mwaka 2007 alijikita zaidi
katika kazi za sheria kupitia sekta binafsi baada ya kustaafu rasmi kazi
Serikalini.
Akizungumza kufuatia uteuzi huo, Mwenyekiti huyo
mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Balozi Muganda amemshukuru Mheshimiwa
Rais Kikwete kwa uteuzi huo na imani aliyokuwanayo kwake na ameahidi kutekeleza
majukumu yake kwa ueledi na uaminifu kwa kadri awezavyo, ili kuiwezesha STAMICO
kutimiza majukumu yake na kuleta tija kwa Taifa.
“Nitaendelea kuwa msikivu kwa
maelekezo na ushauri wa Rais na wa Wizara ya Nishati na Madini katika kutimiza
wajibu wangu wa kuiongoza bodi hii ili iweze kusimamia ipasavyo uendeshaji wa
Shirika, Shirika ambalo ni tumaini kubwa kwa taifa katika uchangiaji wa ukuaji
uchumi na kuondokana na umaskini.” Alifafanua Balozi Muganda.
Amesema kwa kuwa Serikali ni
mmiliki mkuu wa hisa za STAMICO, hivyo kupitia wadhifa huo mkuu atajitahidi
kuhakikisha kuwa Shirika hilo linatoa gawio Serikalini ili kuchangia katika
mfuko wa Serikali na kuleta maendeleo ya Taifa.
“ingawa STAMICO iko katika hatua ya ukuaji katika uzalishaji wa
madini, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika chini ya usimamizi wangu, itahakikisha
inaboresha mbinu za usimamizi wa STAMICO na utekelezaji wa majukumu yake ili kuliwezesha Shirika kufikia dira, mwelekeo
na malengo ya uanzishwaji wake” aliongeza Balozi Muganda.
Amesema katika kipindi chake cha uongozi wa Bodi ya STAMICO, atajitahidi
kuhakikisha kuwa Shirika pia linachangia katika kuongeza nafasi za ajira katika
sekta ya madini na linajenga uwezo wa kiteknolojia
na kifedha kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuchangia katika kukuza uchumi wa taifa.” Alibainisha
Balozi Muganda.
Balozi Muganda amesema
Serikali imempa dhamana kubwa Mtendaji Mkuu wa STAMICO katika kuliongoza
Shirika hilo, hivyo ni matumaini ya Watanzania kuona kuwa Shirika hilo na
wafanyakazi wake wanajituma kwa uadilifu, uaminifu na mshikamano katika
kutekeleza malengo ya Shirika na hivyo kutoa matokeo ya kazi yanayopimika, kwa
wakati muafaka.
Amewataka wafanyakazi wa
STAMICO na wa Kampuni yake Tanzu ya STAMIGOLD, kushiriki katika kukabiliana na changamoto inayoikabili
STAMICO ya kukuza pato la Taifa, kwa kujituma kufanyakazi kwa bidii, kujiepusha
na vitendo vya wizi na kutokomeza ubadhirifu wa mali ya umma, ili kuliwezesha Shirika
hilo kuongeza mapato na kukuza pato la Taifa.
Shirika la Madini la Taifa
lilianzishwa rasmi mwaka 1972 chini ya Sheria ya Mashirika ya umma ya mwaka
1969 kwa lengo la Kusimamia hisa za Serikali kwenye migodi mikubwa nchini; kuwekeza
katika sekta ya madini kupitia utafiti, uchimbaji, biashara na uendelezaji wa
madini; kutoa huduma za uchorongaji, utafiti na ushauri wa kitaalamu kwenye
sekta ya madini na kuratibu shughuli za uendelezaji wachimbaji wadogo ili kuwajengea
uwezo katika uzalishaji wa madini na kuboresha masoko.
Imetolewa na
Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji,
Shirika la Madini la
Taifa,
Plot No 417/418,
UN Road,
S.L.P 4958,
Dar es Salaam,
Tanzania.
Tovuti: www.stamico.co.tz
Barua Pepe: Info@stamico.co.tz
Simu: +255-22-2150029
No comments:
Post a Comment