Thursday, December 25, 2014

TAIFA CUP WANAWAKE KUANZA JANUARI MOSI


TAIFA CUP WANAWAKE KUANZA JANUARI MOSI
Mashindano ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup Wanawake) yanazinduliwa rasmi Januari Mosi mwakani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwa mechi kati ya wenyeji Mwanza na Mara.
Mechi hiyo itakayoonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Azam itachezwa kuanzia saa 10 jioni. Mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Proin yatachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini katika hatua ya kwanza.
Januari 10 mwakani ndipo zitachezwa mechi kwa mikoa yote ambapo Geita itakuwa mwenyeji wa Kagera (Uwanja wa Geita), Tabora vs Kigoma (Ali Hassan Mwinyi), Simiyu vs Shinyanga (Uwanja wa Simiyu), Arusha vs Manyara (Sheikh Kaluta Amri Abeid), na Kilimanjaro vs Tanga (Uwanja wa Ushirika). 
Mechi nyingine ni Lindi itaikaribisha Mtwara kwenye Uwanja wa Ilulu, Ruvuma vs Njombe (Uwanja wa Majimaji), Mbeya vs Iringa (Uwanja wa Sokoine), Katavi vs Rukwa (Uwanja wa Katavi), Dodoma vs Singida (Uwanja wa Jamhuri) na Pwani itakuwa mwenyeji wa Morogoro katika Uwanja wa Mabatini.
Timu hizo zitarudiana Januari 13 mwakani, ambapo baada ya matokeo ya nyumbani na ugenini timu iliyoshinda ndiyo itakayoingia hatua inayofuata ambayo pia itashirikisha mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke.
Hatua hiyo, mechi zake za kwanza zitachezwa Januari 17 mwakani wakati zile za marudiano zitafanyika Januari 21 mwakani.
Baada ya hapo, hatua itakayofuata ni robo fainali, nusu fainali na fainali ambayo ndiyo itakayotoa bingwa wa michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini.
Mdhamini atatoa jezi kwa timu zote zinazoshiriki kabla ya kuanza mashindano hayo.
SDL KUTIMUA VUMBI KRISMASI
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayochezwa katika makundi manne tofauti inaingia raundi ya nne kesho (Desemba 25 mwaka huu) kwa mechi ya kundi C kati ya Kiluvya United na Abajalo itakayochezwa Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani.
Mechi nyingine ya kundi hilo kati ya Mshikamano FC na Transit Camp yenyewe itachezwa keshokutwa (Desemba 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
Kundi A litakuwa na mechi Jumamosi (Desemba 27 mwaka huu) ambayo itazikutanisha timu za Ujenzi Rukwa na Mji Mkuu (CDA) kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga. Desemba 28 mwaka huu ni kati ya Mvuvumwa FC na Milambo SC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Jumamosi (Desemba 27 mwaka huu) kundi B litakuwa na mechi kati ya Arusha FC na Pamba (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha), na Mbao FC vs JKT Rwamkoma (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza).
Kundi D siku ya Jumamosi hekaheka itakuwa kati ya Mkamba Rangers na Volcano (Uwanja CCM Mkamba), Njombe Mji vs Wenda FC (Uwanja wa Amani, Njombe) na Town Small Boys vs Magereza FC (Uwanja wa Majimaji, Songea).

Ratiba ya michuano ya Taifa Cup Wanawake pamoja na msimamo wa SDL vimeambatanishwa (attached).

No comments:

Post a Comment