DAR ES SALAAM
KAMATI
ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA) imemteua Makamu Mwenyekiti wa TASWA, ambaye pia Mhadhiri
Msaidizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma
(SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Egbert Mkoko (pichani),
kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania mwaka
2015/2016.
Pia
TASWA imeteua wajumbe tisa wa kamati hiyo. Majina yao na vyombo vyao
katika mabano ni Mahmoud Zubeiry (Bin Zubeiry Sports- Online), Jane John
(TBC), Baruani Muhuza (Azam Media), Limonga Justine (Redio Uhuru),
Maulid Kitenge (E-FM Redio), Deogratias Rweyunga (Redio One/ITV),
Shaffih Dauda (Clouds Media), Asha Muhaji (Bingwa) na Nelly Mtema (Daily
News).
Kamati
inaweza kuongeza wajumbe wengine au kupunguza kwa kadri itakavyoona
inafaa. Utaratibu wa kuizindua kamati hiyo unaandaliwa na sekreterieti
ya TASWA. Jukumu la kamati itakuwa ni kuandaa utaratibu wa kuwapata
wanamichezo watakaowania tuzo hiyo na pia kuteua washindi kwa kila
mchezo.
Tuzo
za Wanamichezo Bora zinazotolewa kila mwaka na TASWA zimepangwa
kufanyika Agosti 26, mwaka huu, Dar es Salaam zikihusisha michezo
mbalimbali.
ZIARA YA MAFUNZO NAIROBI
TASWA
kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Kenya,
vimeanzisha program ya ziara ya mafunzo na kubadilishana uzoefu baina ya
vyama hivyo viwili, ikiwa katika makundi tofauti ya wahariri/waandishi
waandamizi na kundi lingine la waandishi wa habari chipukizi.
Kwa
kuanzia wahariri wa habari za michezo 18 au wale wenye uzoefu katika
uandishi usiopungua miaka kumi kutoka vyombo mbalimbali vya habari
nchini wataenda Nairobi kwa ziara ya mafunzo kuanzia Julai 6-9 mwaka
huu.
Tunaamini wakirudi wataendelea kuwa waalimu wazuri kwa wale chipukizi, ambao nao watapata fursa kama hiyo siku za usoni.
Imetolewa na :
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
01/06/2016
No comments:
Post a Comment