Friday, August 26, 2016

PSPF YAKABIDHI VIFAA VYA MICHEZO KWA JESHI LA MAGEREZA UKONGA JIJINI DAR ES SALAAM


Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Abdul Njaidi, (kushoto), akimkabidhi seemu ya vifaa vya michezo, Mkuu wa Kikosi Maalum cha Jeshi la Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Rajabu Nyange Bakari, Agosti 25, 2016. Vifaa hovyo ni vya michezo ya ngumi, mpira wa miguu na mpira wa pete.

 Afisa Masoko wa PSPF, Magira Werema, (kushoto), akimkabidhi sehemu ya vifaa hivyo, Mkuu wa Kikosi Maalum cha Jeshi la Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Rajabu Nyange Bakari.


NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
MFUKO wa Pensheni wa PSPF, umekabidhi vifaa vya michezo kwa wanamichezo wa Jeshi la Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam na kasha kufuatiwa na PSPF bonanza la michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, Ngumi na Judo.

Akikabidhi vifaa hivyo vya michezo Agosti 25, 2016, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko huo, Abdul Njaidi, alisema, PSPF imeamua kutoa vifaa hivyo ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua michezo nchini.

“Nyinyi mkiwa kama sehemu kubwa ya wanachama wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, tunayo furaha kutoa vifaa hivi vya michezo kwani baada ya kutekeleza majukumu mazito ya kitaifa mnahitaji kushiriki michezo ili kujenga afya lakini pia kuinua vipaji vyenu,” alisema na kuongeza,

 “Nichukue fursa hii kuwahamasisha mjiunge na PSPF kwani kuna faida nyingi mtapata kutokana na kutoa mafao mbalimbali yatakayoboresha maisha yenu kama ambavyo kauli mbiu yetu inavyosema, PSPF ni chaguo lako sahihi na kamwe hutajutia uamuzi wako wa kujiunga na Mfuko huu.” Alisisitiza Njaidi.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya wanamichezo hao, Mkuu wa Kikosi Maalum cha Magereza-Ukonga, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Rajabu Nyange Bakari, aliishukuru PSPF kwa msaada huo wa vifaa vya michezo kwani vitawawezesha wanamichezo hao kushiriki michezo katika mazingira bora ya kiuanamichezo.

Baada ya makabidhiano hayo, wanamichezo hao walionyesha uwezo wao katika michezo ya mpira wa miguu, ngumi, mpira wa pete, na judo.

No comments:

Post a Comment