Thursday, May 20, 2010
HII MPYA YA MWAKA, WAPEMBA KISA CHA NDOA ZA BARA,NI KOMBORA LA CCM KWA CUF KUELEKEA UCHAGUZI MKUU
ABDALLA ALLY MTOEA MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA TEMEKE KWA TIKETI YA C.U.F
Na Moses Ng’wat
Mbeya.
WAZIRI mdogo mstaafu wa Afya na ustawi wa jamii katika serikali ya mapinduzi Zanzibar, Zainabu Khamis Shomari ametoa tuhuma nzito kwa Chama cha Wananchi CUF kuwa kimekuwa kikiwatuma wanaume wa visiwani Pemba ambao wengi ni wafuasi wake kwenda kuoa na kuhamishia makazi Tanzania bara kwa lengo la kuongeza mtandao wa chama hicho kwa kuwarubuni wanawake hao na majirani zao kuhamia chama chao.
Shomari ambaye pia ni mjumbe wa baraza kuu la CCM Taifa (NEC)na katibu wa CCM wilaya ya Chake Chake amesema wanaume hao wa Pemba ambao wengi ni wafuasi wa chama cha wananchi CUF wamekuwa wakihamishia shughuli zao za uchumi mikoa ya Bara na kuoa wanawake wengine ilhali huko walikotoka wameacha wake kwa lengo la kisiasa ili kujichimbia mizizi kwa kuwarubuni kuhamia CUF.
Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki mkoani Mbeya ,wakati akiwahutubia wajumbe wa Jumuiya ya wanawake wa CCM (UWT) wilayani hapa ikiwa ni moja ya Jumuiya hiyo
kuhamasisha wanawake wa CCM kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki kugombea nafasi za uongozi,pamoja na kupiga kura.
Alisema alibaini mbinu hiyo mpya ya CUF wakati akiwa katika ziara kwenye mkoa wa Lindi na mingine ya pembezoni mwa bahari ya Hindi,ambapo baadhi ya wanaume wa Pemba wamekuwa wakitumia hila kuwadanganya wanawake wa mikoa hiyo kuwa wanawaoa na baada ya muda mfupi huwabadilisha misimamo yao ya kisiasa na kuhamia CUF.
“Wanawake wenzangu naomba niwaibie siri moja ,kaka zangu hawa ni hatari sana katika suala la mapenzi kwani akiwaonjesha mara moja tu huwezi kumuacha ng’o,hivyo basi kuweni makini la sivyo mtajikuta wote mmenogewa na kurubuniwa kirahisi kufuata itikadi zao za kisiasa ” alisema Mrisho huku ukumbi mzima ukilipuka kwa vicheko.
Kadhalika Shomari alifichua kwa kusema kuwa wanaume hao wa kipemba ni waongo kwa kuwa huko walikotoka wameacha familia zao na wake wanne na kitendo wanachokifanya ni kuwarubuni wanawake wa bara
wajiunge na CUF si ndoa kama wanavyodhani wanawake wa Tanzania Bara.
‘’Mie nashukuru nimeolewa na Mndengereko….lakini ningeolewa na Mpemba name ningekuwa katika ndoa ya mitara na pengine kutelekezwa.’’alisema.Alisema wanaume hao hawaishii katika familia zao hizo mpya walizozianzisha kwa hila, bali hutumia mwanya huo kuwa karibu na majirani zao wapya ambao nao huanza kushawishi wa taratibu na hatimaye hukubali na kujiunga na chama hicho.
“Nilipo kuwa Kilwa mkoani Lindi nimeshangaa kuona wanaume wengi wa Pemba wameoa huko na kutengeneza mtandao mkubwa wa CUF,jamani akinamama wenzangu wa bara tusipo kuwa makini tutajikuta tumebadili itikadi zetu na kutekwa kiurahisi kwa sababu ya kukurupukia ndoa za wajanja haa” aliongeza.
Alisema mbinu hiyo haijaishia kwa mikoa hiyo pekee kwani hata alipokuwa mkoani Ruvuma alishuhudia wimbi kubwa la wanaume wa visiwa vya Pemba kuhamishia makazi huko na kuoa wake wa bara ,jambo amblo lisipochukuliwa umakini
na CCM linaweza kuiweka pabaya katika siku za usoni.Aidha,Shomari alienda mbali zaidi kwa kueleza kuwa CUF wamekuwa wakijikita zaidi katika mikoa yenye waislamu wengi kutokana na kluamini kuwa dhana yao hiyo ya kuvuna wanachama wa CCM inaweza kufanikiwa kiurahisi.
Pia aliwatolea uvivu wanawake wenzake wa CCM kuwa kamwe hawawezi kufanikiwa kukamata uongozi katika uchaguzi ujao endapo wataendelea na tabia za kujibagua miongoni mwao kwa kuwa makundi yanayojitokeza ndani ya chama hicho ni sumu kwa chama.
“Jamani mshikamano ndani ya chama ndio silaha muhimu katika upatikana wa ushindi kwenye uchaguzi ujao,wanawake msiendeleze umbeya,Masengenyo na lugha za kashifa kwa wenzenu waliojitokeza kuomba nafasi kwani fursa hiyo ni kwa wote” alisema.
Hata hivyo alisema ameshangazwa na wanawake wa CCM kukubali kuhongwa vitenge na watu wenye nia ya kuomba madaraka katika chama hicho kwani hali hiyo huwafunga midomo na klushindwa kuhoji hata kama watabaini
viongozi waliowachagua wanakwenda kinyume.
Alisema katika hali hiyo si rahisi kwa mwanachama aliyehongwa kitenge kusimama na kumstuta kiongozi wake kwa kuwa dhamira ya kitenge alichopewa humfunga mdomo.
Akizungumzia suala la wanachama wa CUF kuoa wanawake wa bara ikiwa ni moja ya ushawishi wa kujiunga na chama hicho Mbunge wa jimbo la Mkanyageni kwa tiketi wa CUF Mohamed Habib Mnyaa alisema kuwa kauli hiyo ni uzushi wa CCM na kuendeleza ubaguzi dhidi ya wananchi wa Pemba.
Alisema kuwa inashangaza kwa kiongozi huyo kutamka maneno hayo ya kibaguzi ilhali suala la ndoa ni faragha ya watu wawili lakini pia ni jambo la kheri na kwamba kitendo ni ni moja ya mshikamano uliopo baina ya wananchi wa Visiwani na upande wa Bara.
Mnyaa aliongeza kuwa hata hivyo maneno ya kiongozi huyo ni kutapatapa kwa CCM kutokana na kukosa uhakika wa kupata kiti katika kisiwa cha Pemba na kwamba iwapo wamebaini kuwa kuoa wanawake wa bara ni moja ya ushawishi na wao CCM wanayo nafasi ya kwenda Pemba na kuoa wanawake wa huko ili kuwashawishi wajiunge na CCM.
‘’Suala la kuoa si jambo la kuzungumzia…kwani kila mmoja anao uhuru wa kuoa au kuolewa na mtu yoyote bila kujali itikadi yake na mahali alipo iwe upande wa Visiwani au bara…suala hilo halina mantiki ni sawa na kushindwa kisiasa,’’alisema Mnyaa.
Alisema kuwa ipo idadi kubwa ya wazungu ambao wameoa na kuolewa visiwani Pemba na kwamba hata hivyo wazungu walioolewa na kuoa huko hakuna walioshawishiwa kuingia katika chama cha wananchi CUF.
No comments:
Post a Comment