Thursday, May 20, 2010
RUSHWA MICHEZONI,MBOFA WAHONGWA KUMBEBA MGOMBEA WA CCM
Na Mosaes Ng’wat,
Mbozi.
KADA wa chama cha mapinduzi (CCM), Japhet Hasunga, ambaye ameonyesha nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Mbozi Mashariki katika uchaguzi ujao, amedaiwa kukitumbukiza chama cha soka wilaya ya mbozi(MBOFA) katika kashfa ya rushwa.
Habari zilizopatikana wilayani hapa zinadai kuwa kada huyo aliwashawishi kwa kuwapatia fedha baadhi ya viongozi wa MBOFA,waliompatia nafasi ya kudhamini mashindano ya soka yaliyojulikana kama mkombozi ili ayatumie kujitangaza na kujiimarisha kisiasa katika jimbo hilo.
Taarifa za ndani za Chama cha Mapinduzi (CCM)wilayani hapa zinadai kuwa hali hiyo imezua malalamiko miongoni mwa wanachama wa chama hicho hali iliyowalazimu baadhi yao kumuandikia barua katibu wa wilaya, wakimtaka amuadabishe kada huyo kutokaka na kukiuka kanuni za kampeni kwa kuanza kabla ya muda wake.
Awali mashindano hayo yalikuwa yakiendeshwa na chama cha soka wilaya ya Mbozi yalijulikana kama kombe la jimbo na kudhaminiwa na mbunge wa jimbo hilo Godfrey Zambi anayemaliza muda wake,lakini alishatangaza nia ya kutetea kiti hicho.
Inadaiwa kuwa katika hali ya kushangaza MBOFA bila kudhingatia makubaliano waliowekeana na mdhamini wao wa awali mbunge Zambi, waliamua kumpatia kada huyo nafasi ya kudhamini hali iliyotafsiriwa kuwa chama hicho kimeamua kujiingiza kwenye masuala ya siasa na kuwabeba baadhi ya wagombea.
Tanzania Daima ilifanikiwa kupata nakala za barua za malalamiko ya wanachama wa CCM zilizoelekezwa kwa katibu wao wa wilaya na nakala nyingine kwa katibu mkuu Yusufu Makamba wakita hatua zichukuliwe dhidi ya kada huyo kwa kuwachezea rafu.
Katika moja ya barua hizo ambayo iliandikwa 31 januari mwaka huu iliyonukuu waraka wenye kumbukumbu CCM /ond/ 194/ vol ii /112 uliotolewa mwaka jana 2009 mwezi februari na katibu mkuu Taifa CCM ambao umeainisha juu ya namna na mipaka ya watu walioonesha nia ya kugombea nafasi za uongozi katika chama hicho watakavyoweza kukitumikia chama bila kujinufasha katika nafasi walizoomba.
Baadhi ya viongozi wa juu wa CCM wilaya ambao hawakutaka majina yao yawekwe wazi walikiri kuwepo kwa malalamiko hayo yanayokituhumu chama cha soka wilaya kutumiwa na wanasiasa na kwamba hali hiyo ilisababisha mei 17 mwaka huu kamati ya siasa wilaya CCM kukutana na kujadili sakata hilo.
Mwenyekiti wa soka wilaya ya Mbozi (MBOFA),Wiliam Mwamlima alikiri kada huyo kupewa nafasi ya kudhamini,lakini alikana kuhongwa ili kumpatia nafasi hiyo, ambapo alifafanua kuwa mdhamini wa awali mbunge Zambi alishindwa kukidhi vigezo.
“Unajua siasa zinamambo mengi,kifupi ni kwamba sisi tulimuomba wala hakutufuata na kutuhonga, mbunge wetu yeye alidhamini kwa miaka miwili mfululizo lakini hata hivyo hakuweza kukidhi vigezo na kusababisha MBOFA kutumbukia kwenye madeni yaliyotokana na uendeshaji wa mashindano hayo” alifafanua Mwamlima.
Japhet Hasunga anayedaiwa kutumia rushwa ili kupata nafasi ya kudhamioni nay eye kujinufaisha kisiasa alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya hali hiyo,alisema anachokijua yeye ni kwamba aliombwa kudhamini na si vinginevyo.
No comments:
Post a Comment