Monday, May 24, 2010

Makerere yatolewa nje Zain Africa Challenge

Makerere yatolewa nje Zain Africa Challenge

· Kenya sasa kutwaa ubingwa

Na Mwandishi wetu

Chuo Kikuu cha Africa Nazarene cha Kenya kimefanikiwa kufuzu hatua ya fainali ya mashindano ya Zain Africa Challenge baada ya kupata pointi 750 dhidi ya 730 kutoka kwa wapinzani wao Chuo Kikuu cha Makerere kutoka Uganda katika mchuano uliofanyika juzi na kuonyeshwa na kituo cha luninga cha TBC 1.

Mashindano ya Zain Africa challenge ni chemsha bongo ya mtoano ya kimataifa inayohusisha vyuo vikuu kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika.

Katika mchuano wa juzi vyuo vyote vilionyesha umahiri wa kujibu kwa ufasaha na hadi mzunguko wa kwanza unakamiliki Chuo Kikuu cha Africa Nazarene wakiwa na pointi 300 wakati Chuo Kikuu cha Makerere walikuwa na pointi 280.

Katika raundi ya mwisho vyuo vyote vilipata pointi 450 kila mmoja lakini Africa Nazarene waliweza kupata ushindi kufuatia ushindi wa pointi 20 zaidi ya wapinzani wa walizozipata katika mzunguko wa kwanza.

Katika msimu uliopita Chuo Kikuu cha Makerere walikuwa washindi wa pili katika michuano hiyo.

Kwa matokeo hayo Chuo kikuu cha Africa Nazarene kinasubiri kukutana na mshindi wa nusu fainali ya pili itakayowakutanisha Chuo Kikuu cha Egerton na Jomo Kenyatta vyote kutoka Kenya, mchezo utakaofanyika jumapili ya wiki ijayo.

Mshindi wa Zain Africa Challenge kwa msimu huu atapata kitita cha dola za marekani 50,000 na kikombe maalum kutoka Zain.

Watazamaji wa Zain Afrika Challenge bado wanafursa ya kushiriki katika mchezo wa Zain kupitia SMS kwa kujibu maswali yanayoulizwa wakati wa mtoano na kujishindia zawadi ya simu mpya za mkononi aina ya Nokia N97 yenye thamani ya zaidi ya shilingi laki nane.

Ili kushiriki katika mchezo wa ZAC watu wenye simu za mkononi watatuma majibu ya swali litakaloulizwa kwenda namba 15315.

Programu ya Zain Afrika Challenge ni sehemu ya juhudi za Zain zinazolenga kuboresha sekta ya elimu na inadhihirisha dhamira ya Zain ya kuleta Ulimwengu Maridhawa kwa wateja wa Zain.

Jumla ya Vyuo Vikuu 100 kutoka nchi nane barani Africa ambazo ni Ghana, Kenya, Malawi, Nigeria, Tanzania, Uganda na Zambia vilichuana katika mtoano wa kitaifa kabla ya kuingia raundi ya kwanza ya fainali ya mtoano wa ZAC nchini Uganda.

No comments:

Post a Comment